January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mpango ataka maeneo ya vituo atamizi kwa ajili vijana wabunifu

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MAKAMU wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema,Tanzania kuna vijana wenye uwezo mkubwa wa ubunifu unaoweza kubadilisha maisha watu.Kufuatia hali hiyo  ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) itenge maeneo ya kujenga vituo atamizi vya kulelea vijana wenye ubunifu ambazo zinaweza kutatua changamoto katika jamii.

Dkt.Mpango ameyasema hayo jana jijini hapa wakati akifunga na kutoa zawadi kwa washindi wa mashindano ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu yaliyofanyika jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri.

Alisema,ubunifu na uvumbuzi ndiyo njia ya mafanikio katika maisha hivyo lazima wahakikishe eneo hilo la ubunifu linakuwa na tija kwa watanzania na Taifa kwa ujumla. 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo kama Taifa tunapaswa tuangalie  msukumo mkubwa kuhamasisha uvumbuzi  na ubunifu kuanzia  kwenye familia na kwamba , ni muhimu kuhamasisha watoto kupenda sayansi na uhuru wa kutoa mawazo na kufikiri.

Amewataka viongozi  hao kuangalia masuala ya ubunifu katika ngazi ya  shule vyuo na taasisi binafsi, walimu katika ngazi zote wanawajibu wa kuwasaidia wanafunzi kupatia fursa na uzoefu.

Vile vile alisema, Sekta binafsi na wadau wanayo fursa katika kukuza vipaji kwa kuchangia kugaramia mafunzo na tafiti zinazofanyika.“Viongozi serikalini  wapaswa kuwa mfano bora na vinara wa kuhamasisha ubunifu  ,kujenga vipaji na utaalaam na kuwa viongozi wanawajibika kuwatia moyo wataalam hapa nchini.”alisisitiza Dkt.Mpango

Alibainisha kuwa ipo haja ya kujenga mazingira mazuri kwa wabunifu  na kutoa tuzo kwa wanasayansi mbalimbali wanafanya vizuri huku akiagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kujielekeze katika kufanya mapitia ya Sera ya elimu na mitaala yake ili tuongeze wanasayansi nchini, kujenga mazingira kwa wanafunzi wetu kupenda masomo ya sayansi.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Adolf Mkenda alisema suala la sayansi teknolojia na ubunifu ni sehemu ya elimu katika mapana yake, ni elimu inayozingatia ujuzi, ufundi, umakini na umahiri.

Amesema hivi sasa Dunia yote inaeleka kwenye mageuzi katika elimu, kwa Tanzania, ifikapo Septemba mwaka huu watakuwa wameshatoa mrejesho kwa wakuu wao wa nchi, na wako tayari kukamilisha kazi hiyo ifikapo Disemba mwaka huu ili mwakani wakati Dunia inaanza mchakato wao watakuwa wanafanya maamuzi.

Profesa. Mkenda akizungumzia mashinano hayo alisema mashidano ya ubunifu yamefanyika katika mikoa 15 kutoka Tanzania na Zazibar huku wabunifu mahiri 200 wakiendelezwa na wizara na bunifu 26 zimeendelezwa na kufikia hatua ya kuwa bidhaa sokoni.