Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa Wasimamizi wa Afya ngazi ya Mkoa kuacha tabia ya kuvilazimisha Vituo vya kutolea Huduma za Afya kununua dawa kwa washitiri ambao wanawataka wao ili kutatua kero ya uhaba wa dawa katika vituo pindi washitiri hao wanapokuwa na upungufu wa dawa.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Juni 20, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Asia Abdukarimu Halamga katika Bunge la kumi na mbili, Mkutano wa kumi na moja kikao cha 51, Jijini Dodoma.
Amesema, kuna baadhi ya Mikoa wameweka mshitiri (Prime Vendor) mmoja na huku kutoruhusu wataalamu katika vituo kununua dawa nje ya huyo mshitiri, kwahiyo anapokuwa amekosa bidhaa za dawa na vifaatiba kutoka Bohari Kuu ya Dawa au kwa huyo mshitiri, Â inasababisha kuwa na uhaba wa Dawa katika vituo hivyo.
Aidha, amewaelekeza Viongozi wa Afya katika Mikoa kutengeneza biashara huria ili vituo viweze kununua dawa kwenye kwa mshitiri yoyote alietimiza vigezo ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa dawa inayoweza kuepukika.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema, katika kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Serikali imeendelea kuiwezesha MSD mtaji ili iweze kufanya kazi kama Bohari ya dawa badala ya kufanya kazi kama Idara ya manunuzi.
Ameendelea kusema, Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 16 kwaajili ya kutunza na kusambaza dawa kila mwezi, na kueleza kuendelea kusimamia muongozo wa matibabu katika kuhakikisha dawa zinazonunuliwa, kutunzwa na kuandikwa na madaktari zinazingatia muongozo wa matibabu.
Pia, amesisitiza kuwa, Wizara imeendelea kuboresha eneo la maoteo ya bidhaa za afya na kuchukua hatua kwa upungufu unaobainika, huku akisisitiza kuendelea kufunga mifumo ya kielektroniki ili kuimarisha usimamizi wa dawa na kuwezesha dawa kutolewa kulingana na wagonjwa husika.Â
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa