April 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Malasusa ataka hospitali ya Haydom kuombea wafadhili wanaoishika mkono

Na Mary Margwe, Timesmajira Online,Mbulu

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Askofu Dkt. Alex Malasusa, amewataka watumishi wa hospitali ya Kiluther ya Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara,kuhakikisha wanawaombea wafadhili wanaoendelea kuishika mkono hospitali hiyo kwa kutoa misaada mbalimbali.

Dkt. Malasusa amesema wakati akizindua jengo la Mama na Mtoto Hospitali ya Rufaa ya Kilutheri ya Haydom wilayani Mbulu Mkoani Manyara, lenye thamani ya bil.6.5 kwenye Jubilee ya miaka 70 ya hospitali hiyo ambayo ilianzishwa Mwaka 1955.

Ambapo amesema amefurahi kuona kuna Mwakilishi wa Balozi wa Norwegian katika uzinduzi huo,huku akisisitiza wasiache kuziombea nchi kama hizo ambazo bado zinaendelea kuishika mkono hospitali hiyo kwa kufanya kazi pamoja nao.

“Si wote ambao bado wana moyo huo, wengine huwa wanachoka na kutafuta sababu nyingine ya kujitoa katika utoaji wa misaada hiyo ama ufadhili huo,”.

Dkt.Malasusa amesema Wamisionari walipofika Haydom walipeleka habari njema ya wokovu na kuwasukuma kuanzishwa hospitali hiyo mwaka 1955.

“Hospitali yetu hii ya Haydom imeendelea kuboresha miundombinu yake kwa kujenga jengo kubwa na kisasa la Mama na Mtoto Malasusa, hivyo mnatakiwa kutambua kuwa furaha ya kwenda Mbinguni lazima ianzie na hapa duniani na si vinginevyo,”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba wa Hospitali ya Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara Dkt. Paschal Mdoe, amesema hospitali hiyo hutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya za Babati, Hanang’ na Mbulu za mkoani Manyara, wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Mkalama na Iramba mkoani Singida, Meatu mkoani Simiyu na Igunga mkoani Tabora na wilaya zingine mbalimbali.

” Tangu kuanzishwa kwa hospitali hii mwaka 1955 ilikua na vitanda 50 sasa tuna vitanda 420 na ilipopandishwa hadhi mwaka 2010 na kuwa ya Rufaa,inahudumia wagonjwa 105,296 wa nje na 14,020 wa ndani kwa mwaka,” amesema Dkt. Mdoe.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara Michael Semindu,amesema Serikali itaendelea kuajiri wataalamu wapya wa afya na kuwapangia hapo ili kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa jamii.