December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Makundi: Matumizi vibatari, kandili sasa basi

Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi

MPANGO wa matumizi ya taa za kandili, tochi za simu, mishumaa na vibatari katika kituo cha Afya Kyaseni Kata ya Uru Mashariki, Wilayani Moshi umefikia kikomo baada ya Shirika la Umeme nchini (TANASCO) kufunga umeme kituoani hapo.

Huduma hiyo sasa inatoa matumini mapya kwa wakazi zaidi ya 13,000 wa Kata hiyo waliokuwa wakitegemea kupata matibabu ya aina mbalimbali ikiwamo upasuaji wa aina tofauti.

Akizungumza na Mtandao huu, Msaidizi wa Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Emmanuel Makundi amesema, sasa afya za wananchi wa kata hiyo zitaimarika na kuwa na uhakika zaidi ikilinganishwa na miezi michache iliyopita.

“Kipindi cha nyuma wananchi walikuwa wakipata shida ya matibabu ikiwemo upasuaji kutokana na kukosa umeme katika kituo hiki lakini sasa tunaimani kuwa huduma hizi zitaimarika mara dufu, ” amesema Dkt. Makundi.

Mhudumu wa Afya, Matron Temba amesema, huduma ya umeme itasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma kwenye kituo hicho cha Afya kwani sasa wanawake wajawazito na watoto wana uhakika wa kupata huduma bora za afya ikilinganishwa na awali.

“Siku za hivi karibuni tulitekeleza wajibu wetu katika kuwahudumia wagonjwa lakini tulipitia wakati mgumu sana maana kutumia mwanga wa simu halikuwa jambo la uhakika, lakini tunashukuru kwa hapa tulipofika,” amesema Temba.

Msimamizi wa Kitengo cha Ujenzi wa Tanesco Mkoani hapa, Emmanuel Msafiri amesema kuboreka kwa huduma za afya ni matokeo ya Shirika hilo kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme maeneo mbalimbali nchini.

Amesema, tayari TANESCO wameshajenga njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 11 yenye urefu wa kilometa 1.5 pamoja na kuongeza mashine moja kubwa ili kusaidia kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika Kata ya Uru Mashariki.