January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Kiruswa kuwatambua wamiliki wa leseni za madini Songwe

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amefanya ziara ya kikazi Mkoani Songwe ambapo ametembelea shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini kwa lengo la kuwatambua wamiliki wa leseni na kutambua changamoto zao.

Katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe Mhandisi Laurent Mayala ashirikiane na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songwe kukagua na kuzitambua leseni ambazo hazijaendelezwa kwa muda mrefu ili zirudishwe wizarani kwa lengo la kuwapa wachimbaji wadogo wenye uhitaji wa kuchimba.

“Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Afisa Madini naomba mkae muangalie maeneo ambayo yanaviashiria vya madini na yameshikiliwa na leseni za utafiti kwa muda mrefu bila kuendelezwa, mtupe taarifa ili tuyafute na tuwapatie wachimbaji wadogo,” amesema Dkt. Kiruswa.

Aidha, Dkt. Kiruswa amemshauri Mkuu wa Mkoa wa Songwe Omary Mgumba kuwepo na Siku Maalumu ya Maonesho ya Madini katika Mkoa wa Songwe ili kuutangaza Mkoa huo na kuyatangaza madini yanayopatikana mkoani humo.

Imeelezwa kuwa, Mkoa wa Songwe umejaliwa kuwa na aina mbalimbali za madini ambayo ni Madini ya Metali kama dhahabu, fedha, shaba, risasi, chuma, madini ya kimkakati kama Neodymium na Praseodymium, Gesi ya Helium na Ukaa, Madini ya viwandani kama Granite, Marble, chokaa na chumvi, Madini ya Vito kama Fluorite, Mica na Sodalite, Madini ya Nishati kama Makaa ya Mawe na Madini Ujenzi kama Mawe, Mchanga, Moramu na Kokoto.

Akizungumzia mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi, Dkt. Kiruswa ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wote wa madini kuhakikisha wanajitokeza kuhesabiwa ili kuisaidia Serikali kupata taarifa na takwimu sahihi zitakazoiwezesha kupanga mipango sahihi kwa watu wake.

Vile vile, Dkt. Kiruswa amesema ili kudhibiti utoroshaji wa madini lazima tufungue masoko kwenye maeneo ya kimkakati ili wafanyabiashara wasitoroshe kwenda kutafuta masoko sehemu ambayo yanapatikana.

Rais Wetu Mama Samia Suluhu Hassan anataka tuwatafufie wachimbaji wadogo maeneo ya kuchimba ambapo itasaidia wachimbaji wadogo wasiingie kwenye maeneo yenye leseni za utafiti.

Pia, Naibu Waziri ametumia fursa hiyo kuliagiza Shirika la Utafiti la Taifa (STAMICO) kutembelea wilaya ya Songwe kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo ambao wameonekana kuwa na changamoto mbalimbali katika shughuli zao.

Dkt. Kiruswa ameupongeza mkoa wa Songwe baada mafanikio yaliyopatikana kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 ya kuvuka malengo ya makusanyo ya maduhuli kwa kukusanya Shilingi Bilioni 28.65 sawa na asilimia 129.82 ya lengo lote la mwaka mzima.

Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe Mhandisi Laurent Mayala amesema lengo la Mwaka wa Fedha 2021/22 ni kukusanya Shilingi Bilioni 35 ambapo ndani ya miezi nane ya mwanzo (July 2021 hadi Februari, 2022) ofisi imekusanya bilioni 16.9, sawa na asilimia 72 ya bilioni 23.3 tuliyopaswa kukusanya hadi sasa.

Aidha, mauzo katika soko la Madini la Songwe yanaendelea kuongezeka kwani mwezi Disemba, 2021 dhahabu iliyouzwa sokoni hapo ilikuwa kilo113 Matarajio yetu ni kuendelea kusimamia sekta hii ili kulifikia lengo lililowekwa.

Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Omary Mgumba ili kupata taarifa za shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini mkoani humo.