January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Kijaji: bei ya bidhaa imeshuka ukilinganisha na Julai mwaka jana

Na Doreen Aloyce, Timesmajira Online,Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu Kijaji amesema katika mwaka wa fedha ulioanza mwezi Julai 2023 bidhaa mbalimbali zimeshuka bei ukilinganisha na mwezi Julai mwaka 2022.

Akisoma taarifa mbele ya waandishi wa Habari jijini Dodoma juu ya mwenendo wa bei za mazao na bidhaa za vyakula kuanzia Julai 2023 amesema bei zimeshuka na hiyo ni kutokana na juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wake hawaumii.

Mwenendo wa bei za mazao na bidhaa za vyakula hususani mahindi kwa mwezi Julai 2023 kilo moja ni kati ya shilingi 665 na 1,500 ambapo imeshuka kwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na bei ya mwezi Juni, 2023 ambayo ilikuwa ni shilingi 1,550 kwa kilo.

“Bei ya chini ipo katika Mkoa wa Iringa na bei ya juu ipo katika mikoa ya Singida, Pwani, na Kilimanjaro,wastani wa bei ya unga wa mahindi nchini umeshuka kwa asilimia 1.5 kwa mwezi Julai 2023 ukilinganisha na wastani
wa bei ya unga wa mahindi kwa mwezi Juni 2023,”.

Pia amesema mchele kwa mwezi Julai 2023 ni kati ya Shilingi 2,000 na 3,400 kwa kilo ambapo imeshuka kwa wastani wa asilimia 1.4 ikilinganishwa na bei ya juu ya mwezi Juni 2023 ambayo ilikuwa ni kati ya Shilingi 3,450 kwa kilo.

“Bei ya chini ya mchele imepungua kwa asilimia 9.1 sawa na kupungua kwa shilingi 200 ikilinganishwa na bei ya chini ya mwezi Juni 2023 ambayo ilikuwa ni shilingi 2,200 kwa kilo na Mikoa yenye bei ya chini ya mchele ni Katavi na Tabora na kwamba bei ya juu ipo katika Mkoa wa Mtwara,”amesema Dkt.Kijaji.

Pia amesema kuhusu bei ya maharage kwa mwezi Julai 2023 imeshuka kwa asilimia 6.9 sawa na kupungua kwa shilingi 250 ikilinganishwa na bei ya juu ya mwezi Juni 2023 ambayo ilikuwa shilingi 3,600 kwa kilo kwamba bei ya chini inapatikana katika Mkoa wa Songwe wakati bei ya juu ipo katika mkoa wa
Mtwara.

Amegusia bidhaa ya viazi mviringo kwa mwezi Julai 2023 ni kati ya shilingi 850 na 1,600 na kwamba bei haijabadilika ukilinganisha na bei ya chini ya mwezi Juni 2023 ambayo ilikuwa shilingi 850 kwa kilo ambapo bei ya chini ipo katika Mkoa wa Rukwa, wakati bei ya juu ipo katika Mkoa wa Songwe.

Akizungumzia mwenendo wa bei za vifaa vya ujenzi Dkt.Kijaji hususani saruji amesema kuwa aina ya 32.5 kwa mwezi Julai 2023 ni kati ya shilingi 14,125 na 23,250 kwa mfuko wa kilo 50 bei ya juu ya saruji hiyo imeongezeka kwa
asilimia 0.5 huku Mkoa wenye bei ya chini ni Tanga wakati bei ya juu ipo katika Mkoa wa Kagera.

Pia kwa upande wa bei ya nondo milimita kumi kuwa kwa mwezi Julai 2023 ni kati ya shilingi 11,750 na 18,000 ambapo bei hiyo imeonesha uhimilivu kwa kutokuwa na mabadiliko yoyote ya bei ya juu ukilinganisha za bei ya mwezi Julai 2023 na mwezi Juni 2023.

Vilevile mwenendo wa bei za bidhaa nyingine ikiwemo sabuni aina ya jamaa, white wash na MO kwa mwezi Julai 2023 ni kati
ya shilingi 2,800 na 3,900 kwa mche ambapo bei ya chini ipo katika Mkoa wa Arusha wakati bei ya juu ipo katika Mkoa wa Kagera.

Hata hivyo ametoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa zote za viwandani kuongeza
jitihada za uzalishaji wa bidhaa kwa ubora unaohitajika sokoni na kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini.

“Hatutovumilia kuona mzalishaji,
msambazaji au muuzaji wa bidhaa yoyote ile akiongeza kiholela bei ya bidhaa yoyote ile bila sababu ya msingi niwaelekeze kupitia kwenu maafisa biashara wote Nchini
waliopo kwenye Halmashauri zetu kuhakikisha wanasimamia ipasavyo eneo hili la bei za bidhaa kwani ni jukumu letu kuwalinda wazalishaji na walaji.