November 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Kijaji aitangaza Tanzania kimataifa kupitia Islamic Channel

Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira

WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amefanya mahojiano maalumu kupitia kituo cha televisheni cha Islam Channel, kinachorusha matangazo yake kutoka jijini London, Uingereza, kwa lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa na kuhamasisha watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani kutembelea nchini.

Katika mahojiano hayo, Waziri Dkt. Kijaji ameeleza kuhusu utajiri wa vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania, ikiwemo hifadhi za wanyamapori, Mlima Kilimanjaro, fukwe za bahari, utamaduni na vivutio vingine vya kipekee vinavyoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo bora ya utalii duniani.

Aidha, amewakaribisha watalii kutoka Uingereza na mataifa mengine duniani kuitembelea Tanzania na kujionea uzuri wa vivutio vyake pamoja na ukarimu wa Watanzania.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na kituo hicho zinaonesha kuwa wanafikia zaidi ya watazamaji milioni 2 ambao ni watazamaji wa moja kwa moja kwa mwezi nchini Uingereza. Pia wanafikia watazamaji milioni 50 kila mwezi kupitia majukwaa yake ya kidigitali.

Ushiriki wa Waziri Dkt. Kijaji katika mahojiano hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii vya Tanzania katika masoko ya kimataifa, kuongeza idadi ya watalii na kukuza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa.