November 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC.Chikoka awataka vijana kutumia fursa

Na Fresha Kinasa,TimesMajira Online,Mara

SERIKALI wilayani Musoma mkoani Mara imewataka vijana kuamka na kuanza kuzitumia kikamilifu fursa zilizopo ndani ya wilaya hiyo na mkoa huo, ili ziweze kuwabadilishia maisha yao kiuchumi na kijamii na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, Novemba 10, 2026, wakati akifungua Kongamano la Vijana wa Mkoa wa Mara, ‘Key Jana Talks’ lililoandaliwa na Shirika la Action Aid Tanzania kupitia Mradi wa ‘Key Jana Impact.

Chikoka amesema, Mkoa wa Mara umebarikiwa kuwa na fursa adimu ikiwemo madini, ardhi yenye rutuba kwa kilimo na ufugaji, Ziwa Victoria pamoja na fukwe za kupendeza zinazoweza kuleta utalii na biashara kubwa.

Amesema, si vizuri kuona vijana wanatumia muda wao mwingi kwenye mambo yasiyokuwa na tija, wakati kila kona ya Mara kuna fursa inayoweza kubadilisha maisha ya mtu kutoka kuwa maskini hadi kuwa mfanyabiashara mkubwa.

“Nitoe wito kwa taasisi mbalimbali za Serikali, binafsi na wadau wote wa maendeleo Wilayani Musoma, kuendelea kuwasaidia vijana waweze kutumia fursa kujikwamua kiuchumi na kijamii ili wajenge uchumi wao na pia kuchangia maendeleo. Zingalieni fursa na kuzitumia, kuweni wabunifu na pia muwe na uthubutu,”amesema Chikoka.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amelishukuru Shirika la Action Aid Tanzania kwa kuwaleta pamoja vijana na wataalam wa Mkoa wa Mara ili kujadili fursa na changamoto zinazowakabili. Amesisitiza midahalo kama hiyo inawapa vijana mwanga, ari na morali mpya ya kubadilisha mawazo yao na kuchangamkia fursa zilizopo.

Kwa upande wake, Arif Fazel kutoka Shirika la Action Aid Tanzania, amesema shirika hilo linaendelea kutekeleza mradi wa “Key Jana Impact” katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Ndani ya mradi huo kuna programu maalumu iitwayo ‘Key Jana Talks’, ambayo lengo lake ni kuwaleta pamoja vijana na wataalamu ili wazungumzie fursa mbalimbali.

Fazel amesema, mbali na fursa, pia kujadili vikwazo vinavyowakabili vijana ili kuvitatua, na kuhakikisha wanatumia fursa kikamilifu kubadilisha maisha yao na jamii kwa ujumla, hususan kubadili changamoto kuwa fursa za kipato endelevu.

Ameongeza kuwa, kupitia mradi huo, shirika hilo limeweza kufanya midahalo katika mikoa ya Ruvuma Wilaya ya Songea, Kigoma, Pemba na Musoma, ili kuhakikisha vijana wanabadili fikra zao na kutumia vyema fursa. Huku akisema lengo ni kuwafikia vijana wengi zaidi nchini.

Amesema, shirika hilo limeendelea kuwasaidia vijana wa Kitanzania katika kuwawezesha kunufaika na uchumi wa buluu na kijani, masuala ya mabadiliko ya tabianchi, kilimo na teknolojia, ili waweze kuinuka na kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Neema Marwa, mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, ambaye ni miongoni mwa vijana walioshiriki katika mdahalo huo, amesema kuwa, anaamini maarifa na ujuzi ulioupata utamsaidia kubuni mbinu bora za kuanzisha mradi mdogo wa ufugaji wa kuku utakaompa faidia tofauti na ufugaji wa mazoea.