December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Jingu: Maandalizi ya Sensa yafikia asilimia 80

Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Dar es Salaam

Kamati ya Ushauri ya Sensa imesema kuwa maandalizi ya kukamilisha zoezi la Sensa kwa mwaka 2022 yanaenda vizuri na tayari yamefika asilimia 80 kwa maeneo yaliyotengwa pamoja na maandalizi ya vifaa vitakavyotumika katika zoezi hilo.

hayo ameyasema leo (Mei 26,2022) Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Sensa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, bunge na Uratibu, Dkt. John Jingu wakati alipokutana na Wawakilishi wa Sekta Binafsi na Wafanyabiashara kuelekea katika zoezi hilo, na kuuongeza kuwa kazi ya kukamilisha na kufanikisha zoezi hilo kwa asilimia zote 100% inaendelea sehemu mbalimbali nchini bila kuchoka.

“Kuna hatua kadha wa kadha tayari tumekamilisha, mwaka jana tulifanya majaribio ya Sensa, na tunaendelea kufanya maandalizi, maeneo tayari yametengwa na vifaa vinaendelea kununuliwa na kazi kwa ujumla inaendelea vizuri, hatuwezi kupumzika hadi siku ya mwisho ya zoezi Agosti 23, 2022”, ameeleza.

“Najua mtajiuliza juu ya ushiriki wa Sekta Binafsi na Wafanyabiashara nchini katika zoezi hili, kwa hakika Sensa hii itawasaidia kupanga Soko lao na bidhaa zao wanazozalisha sehemu mbalimbali nchini, itawasaidia kujua idadi ya watu na rika ili watoe huduma zinazostahili kwa watu hao”, amesema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu amesema Wafanyabiashara na Sekta Binafsi wanapaswa kufanyia kazi wito wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukamilisha zoezi hilo kwa kusaidia kuweka Matangazo ya Nembo ya Sensa kwenye bidhaa mbalimbali kama inavyofanya Serikali kutangaza zoezi hilo na kuhamasisha nchi nzima kupitia masuala yake mbalimbali.

Aidha Mwenyekiti huyo amesema ni bahati kwa mwaka huu kupata fursa ya kufanya sensa kwasababu itasaidia kujua soko la bidhaa na kupanga mipango ya kibiashara;

“Sensa hii itakua ni sensa ya sita tangu nchi yetu ilivyoanza hivyo ni jambo kubwa ambalo linafanyika kila baada ya miaka 10 na mwaka huu tunabahati ya fursa ya kufanya sensa ya kitaifa”

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza kutoka Zanzibar ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Thabit Faina amesema Suala la uhamasishaji wa sensa linakwenda vizuri kwa kiasi kikubwa na sasa wamebakisha hatua ndogo ya 20%.

Pia Faina amesema Matarajio yao ni kuona wapi panahitaji huduma ya Afya, kujenga shule mpya, kuwekeza aina ya biashara mbalimbali katika maeneo tofautitofauti

Mbali na hayo Mwenyekiti Mwenza huyo amesema ni vyema kwa muda uliopo kukamilisha suala la sensa kwa kuendelea kushirikiana vyema na wafanyabiashara;

“Tuhakikishe muda huu ambao tulionao kuona tunalikamilisha hili kwa ufanisi mkubwa na tunaimani kubwa na wafanyabiashara kwasababu ni wadau wakubwa katika kulifanikisha jambo hilo la sensa”

Akizungumza kwa niaba ya Sekta Binafsi, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, Paul Makanza amesema kupitia zoezi hilo la Sensa, Sekta binafsi itafaidika na takwimu hizo za idadi ya watu na makazi na kuzifanyia kazi ipasavyo hususani katika Sekta ya Biashara kulingana na uhusiano wa Sekta hiyo na idadi ya watu.

“Sisi Sekta Binafsi tunawapongeza sana kwa hatua mliofikia hadi sasa kuelekea kukamilisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi nchini, sisi tunaunga mkono zoezi hili la kupata takwimu za Watu na Makazi kwa nchi nzima”, amesema Makanza.

Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 itakuwa Sensa ya Sita tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine ziliwahi kufanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012, zoezi hilo linafanyika kila baada ya miaka 10.