Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Serikali imeendelea na juhudi za kuimarisha mazingira ya biashara nchini kwa kuboresha miundombinu na kuwekeza katika sekta za usafirishaji na kilimo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt.Selemani Jafo,ameeleza hayo Septemba 10, 2024, wakati wa kufungua maonesho ya 19 ya Afrika Mashariki, yanayofanyika uwanja wa Furahisha, wilayani Ilemela mkoani Mwanza, kuanzia Septemba 6 hadi 15 mwaka huu, yaliyoandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).
Dkt.Jafo amebainisha kuwa Serikali imeagiza kila Mkoa kujenga viwanda 30 kila mwaka, ikiwa ni pamoja na viwanda vikubwa 5, vya kati 5, na vidogo 20. Hatua hii inatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 100,000 kwa mwaka.
Jafo amesema kwamba Serikali imeongeza bajeti ya kilimo kutoka bilioni 294 mwaka 2021 hadi tirioni 1.2 bajeti ya mwaka 2024/2025, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha kilimo cha umwagiliaji na kupunguza utegemezi wa mvua.
Kuhusu miundombinu, Serikali inaendelea kuwekeza katika barabara, usafiri wa anga, na reli, ikiwa na ndege 15 na treni ya umeme inayounganisha Dar-es-Salaam na Dodoma, na ujenzi wa reli wa kisasa unaendelea hadi Mwanza na Kigoma.
Aidha, Serikali imewekeza katika kuboresha bandari, ikiwa ni pamoja na bandari za Dar-es-Salaam, Mwanza Kasikazini,Kemondo, na bandari nyingine kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.Pia ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametanua wigo wa biashara na masoko, huku wananchi wa Kitanzania wakipata fursa ya kuuza bidhaa Marekani, China, na Afrika Mashariki.
“Wizara ya Viwanda na Biashara,hivi karibuni tumezindua sera ya biashara ya mwaka 2025, lengo ni kuhakikisha wafanyabiashara wengi wanapata fursa ya uwekezaji na kufanya biashara katika maeneo mengine, ikiwemo soko la China ambayo ni fursa ya Watanzania katika kujenga uchumi,”.
Sanjari na hayo Jafo aliwahimiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya, na Halmashauri kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya viwanda na masoko.Amesisitiza kwamba ujenzi wa miundombinu ya kudumu ni muhimu kwa mafanikio ya biashara.
Vilevile Dkt.Jafo,ameitaka TCCIA,kufanya maonesho kama hayo kwa ngazi ya kitaifa,ili kupanua wigo wa wafanyabiashara kufanya biashara,kuongeza mtandao wa kibiashara(network),ili nchi iweze kusonga mbele na watu wapate taarifa za kibiashara na masoko na kuweza kusajili biashara zao.
Awali Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene, alimuomba Waziri Jafo kusaidia kupata kiwanja cha kudumu kwa maonesho ya kibiashara.
Kenene pia ameeleza changamoto ya utitiri wa kodi na kuomba Serikali kupunguza mzigo huo ili wafanyabiashara waweze kustawi na kulipa kodi kwa urahisi.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais