January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Hashil apongeza utendaji wa Brela Sabasaba

Na Penina Malundo, timesmajira

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdalah amepongeza utendaji kazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), katika Maonesho ya 47 Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere, Temeke Dar es Salaam.

Hayo yamejiri jana alipofika katika banda la Taasisi hiyo lililopo nje ya jengo la Wizara ya Fedha na kuona wadau mbalimbali wakipatiwa huduma za papo kwa papo na kukabidhiwa vyeti vya usajili.

“Nimefurahishwa na mwitikio wa wadau wengi waliokusanyika katika Banda hili na ikiwa ni miongoni mwa Taasisi chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara mnafanya kazi nzuri na kuiwakilisha vyema Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan”, ameeleza Abdallah.

Ameongeza kuwa amefurahishwa sana kuona wadau wengi wamefika kusajili Majina ya Biashara, Kampuni, kusajili Alama za Biashara na Huduma, Kupata Leseni za Biashara Kundi “A” na Leseni za viwanda na huduma zingine kutoka BRELA ambazo zinatolewa papo kwa papo na kueleza kuwa BRELA inaiwakilisha vyema Wizara katika maonesho hayo.

Dkt. Abdallah amewataka wadau ambao wanafika na kupata huduma katika mabanda ya BRELA kuwa mabalozi na kuwaleta wadau wengine kupata huduma za kuramisha Biashara zao.

Aidha, amewataka watumishi wa BRELA kuendelea na kasi ya utendaji kazi ili kuleta matokeo chanya ya kuwezesha Biashara kwa kuzingatia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI).