November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Gwajima ayataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuelimisha jamii kuhusu chanjo ya UVIKO 19

Na Na Joyce Kasiki,Dodoma,timesmajira,online

WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia na Watoto Dkt.Doroth Gwajima ameyataka Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCongo) kufanya kazi zao kwa uwazi na weledi ili kufanikisha azma ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha ameyataka mashirika hayo ,kutumia nafsi yao katika kuwaelimisha wananchi kuhusu chanjo ili wapate huduma hiyo kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19.

Dkt.Gwajima ameyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa NaCongo uliofanyika jijini hapa.

“Wakati mnapofanya kazi zenu mhakikishe mnafanya kazi kwa uwazi ,weledi,uadilifu na uzalendo wa hali ya juu  ndipo shughuli zenu zitaleta tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.”amesema Dkt.Gwajima na kuongeza kuwa

“Pia mnalo jukumu la kuhakikisha mnatoa elimu kwa wananchi kuhusu chanjo ili kuwezesha wananchi kuelewa kuhusu chanjo ya UVIKO 19  na hatimaye kujitokeza kupata chanjo hiyo kwa hiyari kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan

Amesema wapo baadhi ya wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu chanjo hivyo wanahitaji kupata elimu hiyo ndipo wajitokeze kwa hiyari yao wenyewe na siyo kwa kutumia nguvu.

“Nia ya Rais Samia ni kuona Taifa lipo salama,mkasimamie na kuwapa wananchi elimu ya kutosha ili kampeni ya chanjo itekelezeke kwa wananchi wote kupata chanjo hiyo.”amesisitiza Dkt.Gwajima

Aidha Dkt.Gwajima amesema mkutano huo ni fursa kwa NaCongo na Serikali kujadili kwa pamoja mipango ya nchi na kuona namna ya kuitekeleza kwa pamoja ili kufikia azma ya Serikali ya mkuwaletea wananchi maendeleo.

 Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mwanaidi Khamis alisema chanjo ya UVIKO 19 ni salama hivyo wananchi wahamashishwe kuchanja.

“Chanjo hii ni salama hivyo ninyi mashirika yasiyo ya kiserikali mnapaswa mkaelimishe wananchi ili wachanje kwa maslahi yao binafsi na Taifa kwa ujumla “

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii  Dkt.John Jingu aliyataka mashirika hayo kutumia mkutano huo katika kujadili na kubaini mafanikio na mapungufu yalioyojitokeza kipindi kilichopita ili kuyatafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa NaCongo Dkt.Lilian Badi alisema,Baraza hilo limekusudia kuelimisha sekta ya NGO’s ili iweze kuiletea nchi Maendeleo.