January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Gwajima aiomba jamii kutoa ushirikiano kwa wadau wanaosaidia kupambana na ukatili dhidi ya watoto

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima ameiomba jamii kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau wote wanaosaidia kupambana na ukatili dhidi ya watoto likiwemo Jeshi la Polisi, Mahakama na Taasisi zinazojihusisha na uboreshaji wa huduma za Madawati ya Jinsia kwa kudhibiti ukatili dhidi ya watoto wadogo.

Amebainisha hayo leo Tarehe 02, Desemba 2021 katika ufunguzi wa Kituo cha Kulea Watoto cha pamoja cha huduma ya mkono kwa mkono kwa watoto waliofanyiwa ukatili kilichopo Chuo Kikuu Kishiriki cha SAUT, Jordan kilichopo Morogoro kitakacho hudumia wananchi wa kata 15 katika manispaa ya Morogoro. Lengo ni kumuwekea kinga mtoto dhidi ya ukatili na kumpa huduma zote pindi anapofanyiwa ukatili.

Dkt.Gwajima amesema kuwa jamii ikitambua umuhimu wa kulea watoto kutapunguza ukatili dhidi ya watoto. Kwa takwimu za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huduma dhidi ya ukatili kwa watoto imeendelea kutoa huduma katika vituo 17 vya mkono kwa mkono hapa nchini na katika kipindi cha Julai 2020 hadi juni 2021 kulikuwa na waathirika 1,857 wa kufanyiwa ukatili wa kijinsia na kati yao watoto 1,072 walihudumiwa” amesema Dkt.Gwajima

“Tatizo la ukatili linaathiri maendeleo ya Taifa kwa kuwa na watoto watakaojifunza ukatili hali inayo ongeza mzigo kwa jeshi la polisi ambalo linafanya kazi kubwa ya kuanzisha madawati ya kijinsia kwa lengo la kuelimisha jamii itambue umuhimu wa kuzingatia maadili na malezi bora kwa watoto ili kuandaa taifa la vijana wazalendo kwa manufaa ya Taifa.

Dkt Gwajima amevipongeza vvyombo vyote vya sheria vinavyoshughulikia masuala ya ukatili na ametoa rai kwa vyombo hivyo vikiwemo polisi na mahakama kuongeza kasi ya kudhibiti kufanyia kazi mashauri ya ukatili ili kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake kwa wakati kwa wale wote wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Awali Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela akimkaribisha waziri wa Afya Dkt Gwajima amesema kuwa Mkoa wa morogoro unakabiliwa na changamoto ya uwepo wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ambapo Jeshi la Polisi kwa Julai hadi Septemba 2021 limepokea taarifa za unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wazima 200 kati yao wanaume wapo 41 na wanawake 159 huku taarifa za watoto 275 zikitajwa kati yao 64 ni wavulana na watoto 136 watoto wa kike hali inayoonyesha watoto wa kike na wakina mama kuwa kwenye mazingira magumu kiasi cha kuhitaji kuimarisha kamati ya ulinzi na usalama ziweze kuweka mikakati madhubuti ili kukabiliana na hali hiyo.

Mkuu wa Chuo Kishiriki cha Jordan Prof.Bertram Mapunda amesema kuwa chuo kimebaini morogoro ukatili upo kwa kiwango cha asilimia 60 ambapo kila watoto 10 sita hufanyiwa ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo ulawiti,Ubakaki,Vipigo,Kuunguzwa kwa maji na moto watoto pindi wanapokosea,kuwafanyisha kazi ngumu,Kuwanyima Chakula,Haki ya kupata elimu,Matibabu na malezi Bora kutokana na ugomvi wa wazazi,Ulevi uliopindukia na msongo wa mawazo hali inayohatarisha maisha ya watoto wadogo