December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Chana:Wafugaji acheni kuingiza mifugo kwenye hifadhi za misitu

Na Zena Mohamed,TimesMajiraOnline,Dodoma.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt.Pindi Chana amewataka wafugaji kuacha tabia ya kuingiza mifugo katika hifadhi ya misitu na hasa katika miti iliyopandwa leo.

Ameeleza kuwa mifugo inachochea jangwa na kupelekea athari ambazo zinafika mbali zaidi na kupelekea hata kutokea kwa upungufu wa maji kwani kunakuwepo na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Waziri Chana amesema hayo jijini hapa leo,Januari 11,2023,wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza katika zoezi la upandaji Miti katika Bwawa la Swaswa lililopo kata ya Ipagala Jijini Dodoma , Ikiwa ni muendelezo wa upandaji miti kuelekea kilele cha Maadhimisho ya miaka 59 ya mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa kuna misitu hekta mil.48.1 ambapo asilimia 30 ni misitu inayomilikiwa na serikali na mingine na taasisi mbalimbali ,hivyo basi tukiilinda miti na yenyewe itatulinda.

“Misitu inatunzwa kwa sheria zilizowekwa kwahiyo ni marufuku kuingiza mifugo katika maeneo yamisitu,lakini pia swala zima la moto hivyo shughuli mbalimbali za binadamu hivyo tusiandae mashamba kwanjiaya moto hivyo basi tutumie njia mbadala,”amesema Dkt.Chana.

Vilevile Waziri huyo amepiga marufuku tabia ya Wakulima nchini kuandaa mashamba kwa kuchoma moto badala yake watumie njia mbadala ili kuendelea kutunza hifadhi Misitu.

Ambapo amesema kuwa wakulima wamekuwa wakitumia njia hiyo kuandaa mashamba yao kuelekea msimu wa kilimo jambo ambalo limekuwa likileta athari katika misitu na uoto wa asili.

Ameeleza kuwa moto huwa una tabia ya kusambaa kulingana na uelekeo wa upepo na kwenda maeneo ambayo hayakukusudiwa kuchomwa hivyo inapelekea uharibifu wa misitu kwani wakulima huchoma moto na kuondoka.

“Wakulima wamekuwa wakitumia njia ya kuchoma moto kuandaa mashamba yao kuelekea msimu wa kilimo jambo ambalo limekuwa likileta athari katika misitu yetu,

Na kuongeza “Tuache kutumia njia hiyo kuandaa mashamba ili kunusuru misitu yetu,”amesema Dkt.Chana

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Abdallah Mitawi alisema kuwa mapinduzi ya Zanzibar ndiyo Kielelezo cha Muungano,Uhuru na Mshikamano wa Tanzania na imeonekana ni vyema kusherehekea kwa kupanda miti ili kuendelea kukijanisha Dodoma.

Amesema kuwa wamedhamiria kupanda miti elfu tano ndani ya siku tatu katika Jiji la Dodoma jambo ambalo litaacha kumbukumbu ya kudumu ya miaka 59 ya mapinduzi ya Zanzibar

“Kupanda miti sio kazi ila kazi kubwa ni kutunza miti hii ikue kwani baadhi ya watu hawana desturi ya kutunza miti hivyo niwatake wananchi kutunza miti na kuacha tabia ya kuachia mifugo kula miti waache mara moja,”amesema Mitawi

Naye  Diwani wa Kata ya Ipagala Gombo Dotto alisema kuwa wao mpaka sasa wamepanda miti 17,000 katika kata hiyo  huku wakiwa na lengo la kupanda miti 50,000 katika msimu huo.

“Miti hii tuliyoipanda tutaitunza na tutaifatilia ,ingawa kunachangamoto za miti ikiwemo kuliwa na wadudu,wananchi kulisha  mifugo yao kama Mbuzi na Ng’ombe hivyo nitoe marufuku kupitisha mifugo kula miti hivyo nikikuta miti imeliwa basi huyo Mbuzi au ,Ng’ombe basi msahau”amesema.

Pamoja na hayo amemtaka Mtendaji kusimamia maeneo na kutaka kila mti uliopandwa na kila mtu basi uwekewe alama na uandikwe jina lake nakuzungushia nailoni  ili ule mti uendelee kutunzwa kwa heshima na mtu aliyepanda,ili tupate nafasi baada ya miaka miwili mitatu tuje tumuonyeshe mti wake jinsi unavyokuwa.