January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko: Matumizi Nishati safi ya kupikia yaanza rasmi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza rasmi nchini ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali kuhakikisha kuwa wananchi hasa kina mama wanahama kutoka matumizi ya nishati ya kupikia isiyo safi kwenda kwenye nishati iliyo safi na salama.

Dkt. Biteko amesema hayo leo tarehe 7, 2024 wilayani Temeke Mkoa wa Dar es Salaam, wakati wa hafla ya ugawaji mitungi ya gesi na majiko banifu kwa wajasiriamali katika Soko la Temeke Stereo na Mbagala- Zakhem.

“Nataka niwaeleze kuwa, safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza katika wiki hii ambayo tunasherehekea siku ya Wanawake Duniani.

“Sababu kubwa ya kufanya hivi, tunafahamu kwamba Mwanamke ni mwathirika mkubwa nishati isiyo safi ya kupikia na wanapata madhara mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa kifua, kubakwa na kutumia muda mrefu kutafuta kuni.

“Hivyo, Serikali imeona kuwa ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi ili kumwezesha mwanamke kupata nishati safi na kwa gharama nafuu,” Amesema Dkt. Biteko.

Amesema, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia siyo tu kwa Tanzania bali Afrika nzima na ulimwenguni.

Na hilo limethibitika wakati akizindua Programu ya Nishati safi ya kupikia itakayosaidia Wanawake Barani Afrika (African Women Clean Cooking Support Programme (AWCCSP) katika Mkutano wa Cop 28 Dubai ambayo imeungwa mkono na wadau mbalimbali hivyo kama nchi lazima iwe na mpango maalum wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameongeza kuwa, zoezi hilo la ugawaji wa mitungi ya gesi na majiko banifu halitaishia Dar es Salaam, bali ni endelevu na litafanyika katika mikoa mbalimbali nchini, ili wananchi katika maeneo yote wahamasike kutumia nishati safi ya kupikia.

Dkt. Biteko ametoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wa Dini, Serikali, Jadi na makundi mengine kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia huku akisisitiza kuwa ajenda hiyo isiwe ya Serikali pekeyake.

Pia, ameomba wadau zaidi wajitokeze kuungana na Serikali katika suala hilo kama ilivyo kwa kampuni ya Oryx ambayo imeonesha kwa vitendo kuwa inaiunga mkono Serikali kwenye nishati safi ya kupikia.

Aidha, amezitaka Taasisi kama vile Shule, Magereza na Hospitali watumie gesi kwenye matumizi ya kupikia na kuanza kubadilisha mifumo ya matumizi ya kuni kwenda kwenye Gesi ili kufanikisha ajenda ya Serikali ya Matumizi ya Nishati safi ya kupikia.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akigawa mitungi ya gesi kwa Wajasiriamali katika eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam ikiwa ni uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Dkt. Biteko pia, amesisitiza utunzaji wa mazingira na misitu ili kuweza kupata maji ya uhakika, umeme na masuala mengine yanayotokana na utunzaji wa mazingira na kueleza kuwa ili vizazi vijavyo visiishi kwenye jangwa ni lazima kuchukua hatua sasa za kuzuia uharibifu wa mazingira.

Kutokana na hilo, ameagiza wasimamizi wa Misitu nchini ikiwemo Halmashauri na Serikali za mitaa kujikita kwenye uhifadhi na utunzaji wa mazingira badala ya kusubiri kukamata mkaa.

Amesema, kila mtu lazima atimize wajibu wake, kuacha tamaa ya kupata fedha kidogo kwa gharama ya mazingira na kwamba jambo la kulinda mazingira na misitu ni jambo la lazima.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema, hali ya upatikanaji umeme nchini ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, inaendelea kuimarika na kwamba kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kuna changamoto ya miundombinu ya kusafirisha umeme lakini Serikali inatenga fedha za kuimarisha miundombinu hiyo ambapo laini ya umeme kutoka Gongolamboto kwenda Mbagala inaimarishwa kwa kujenga laini kubwa zaidi ya umeme na pia transfoma iliyopo Mbagala yenye ukubwa wa MVA 50 inabadilishwa na kuwekwa ya MVA 120.

Amesema pia, inajengwa laini ya umeme chini ya ardhi ya kilometa 6 kutoka Kurasini kwenda Ilala ambayo itapunguza mzigo wa laini ya Mbagala na hivyo kufanya upatikanaji umeme kuwa tulivu na himilivu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amemshukuru Dkt. Biteko kwa maono yake ya kuhuisha azma na maono ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia na pia kuendeleza kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Amesema kuwa, tukio la jana ni mwendelezo wa matukio yaliyopangwa kutekelezwa na Wizara ya Nishati ambapo tarehe 9 Machi, 2024 Wizara ya Nishati itaendesha kongamano kubwa la Wanawake takribani 4000 kutoka Wilaya na Mikoa yote nchini ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kapinga amesema kuwa, asimilia 63 ya wananchi nchini wanatumia kuni kwa ajili ya matumizi ya kupikia, asilimia 25 wanatumia mkaa na asilimia takriban 5 wanatumia nishati mbadala kama Gesi, hivyo safari bado ni ndefu kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia na kwamba azma ya Rais ya asilimia 80 ya Wananchi kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033 itafikiwa.

Amesema, ugawaji wa vitendea kazi hivyo ni mwanzo tu kwani zoezi hilo litafanyika nchi nzima kadri rasilimali zitakavyopatikana kwani lengo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameishukuru Wizara ya Nishati kwa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa mitungi hiyo ya gesi ambayo ameeleza kuwa itasaidia kuondoa ukataji wa miti hovyo, kulinda dunia pamoja na ikolojia iliyopo.

Pia, amepongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Nishati kupitia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambazo zimepelekea changamoto ya umeme kupungua kwa asilimia 85 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo Mbagala.

Kwa upande wake, Katibu wa Mama Lishe, Soko la Temeke Stereo, Mwanahamisi Nditi ameshukuru Serikali kwa kupata mitungi ya gesi na majiko banifu ambayo itawawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi kwenye soko hilo na kueleza kuwa matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa na changamoto kwao kutokana na kufanya kazi kwenye moshi mwingi ambao unaathiri afya zao.

Pia, ameomba kuwa zoezi hilo liendelee kutokana na uwingi wa mama lishe katika soko hilo ambao ni takriban 78  na wasaidizi wao wapatao 70.

Viongozi wengine waliofuatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati katika hafla hiyo ya ugawaji wa mitungi ya gesi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. James Mataragio.