November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko azindua Sera Taifa ya Biashara

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka watumishi Serikalini kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na misingi ya utoaji wa huduma ili kuleta matokeo Chanya na sio kuwakwamisha watu wanohitaji huduma.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo (Julai 30,2024) wakati akizindua Sera Taifa ya Biashara katika hafla iliyofanyika Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Serikalini na sekta binafsi.

Amesema katika baadhi ya ofisi kuna watu mahiri wa kuandaa maandiko lakini utekelezaji wa majukumu yao hauna uhalisia na hauendani na nyaraka walizoziandaa na hivyo nyaraka hizo kubaki kwenye makablasha.

“ Tunaweza kuwa wazuri sana wa kuandika kutoa matamko na kutoa ahadi lakini hali halisi haibadiliki, Hakuna faida ya kuwa na afisa anayejipanga kumkwamisha mfanyabiashara ili tu aitwe bosi, Tunatakiwa kuwa na nyaraka inayotuunganisha wote vinginevyo sera hii itabaki kuwa kitabu cha hadithi kwenye kabati,” Amesema Dkt.Biteko

Amewahimiza watumishi serikalini kuwahakikishia watu wote wanapata huduma hizo pasipo kuwekewa vikwazo suala ambalo litawajengea heshima mbele za watu wanaotafuta huduma hizo, “Uwepo wa sera ya taifa ya Biashara utasababisha mabadiliko makubwa katika nyaraka na sheria mbalimbali za nchi na hivyo sekta zote za serikali zinatakiwa kuisoma sera hii na kuisimamia.“ Amesema Dkt. Biteko

Katika hate nyingine, Dkt. Biteko amewataka watanzania kutumia fursa ya Sera hii kuwa nyezo ya kuimarisha nguvu za kiushindani kitaifa, kikanda na kimataifa huku akiainisha hifadhi ya mazingira na kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Aidha amewataka watanzani kutembea kifua mbele wakiamini kuwa wanao uwezo wa kushindana na kushindanisha bidhaa kwa kuboresha bidhaa hizo ili kuvutia masoko ya ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia kuwa sera hii ni ya biashara na siyo sera ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Dkt. Biteko pia amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan haipendi kuona ama kusikia kero dhidi ya wafanyabiashara hivyo, wadau wote wana ni umuhimu kutumia fursa hiyo kuboresha huduma kupitia sera hii mpya.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe, Dkt. Selemani Jafo amesema mabadiliko ya kibiashara duniani yanasababisha mabadiliko ya biashara na mitaji kuwawezesha watanzania kushiriki katika ujenzi wa Uchumi huku akiwashukuru wadau wa maendeleo kwa mchango wao katika maandalizi ya Sera hiyo.

Awali akitoa salamu za Bunge na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mariam Ditopile ameipongeza Serikali kwa hatua ya kupata sera hiyo na kushauri kwa kuwa na uratibu wa pamoja katika masuala yanayoendana na kuondoa urasimu unaosababisha kukosekana kwa tija.

Kwa upande wake, Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Tone Tinnes amesema ni wazi kuwa Tanzania imekuwa kivutio cha biashara na imeongeza mauzo ya bidhaa zake poamoja na uwekezaji wa mitaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchini.

Amesema suala la manufaa zaidi ni uwekezaji katika kuboresha masuala ya jinsia, vijana na hifadhi ya mazingira.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binfasi nchini (TPSF), Raphael Maganga amesema serikali imeonesha nia na nguvu ya kimfumo katika kusimamia biashara kwa kuunganisha uratibu wa biashara na kuja sera inayolenga kuwaunganisha wahitaji na kuunganisha wafanyabiashara wadogo na wale walio katika sekta rasmi.

Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Biashara umebeba Kaulimbiu Ushindani wa Biashara katika kuchochea kasi ya mabadiliko ya Jamii ya kiuchumi yanayoongozwa na viwanda.