April 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Biteko ataka jamii kuenzi Falsafa za Baba wa Taifa

Na Rose Itono,Timesmajira

NAIBU Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko amewataka watanzania kuenzi mambo ya msingi aliyoyasimamia Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kujifunza umuhimu wa amani kwa kuilinda kwa gharama yeyote

Akifungua Kongamano la Kumbukizi ya Siku ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) Dar es Salaam Jana Dkt. Biteko alisema hakuna Taifa lolote kinaloweza kupata maendeleo pasipo kuwa na amani

Dkt. Biteko amesema enzi za uhai wa Hayati Mwalimu Nyerere alipanda mbegu ya amani ambayo mataifa mengi walitamani kuwa nayo,na kupitia falsafa hiyo yeyote atakayezungumzia uvunjifu wa amani apuuzwe

Amewataka vijana kufanya tafakuri ya mambo ambayo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyaamini na kuyaishi kwa kujifunza kupitia makongamano ya aina hii ili kudumisha amani na umoja wa kitaifa

Amesema kwa kuendeleza fikra hizo ipo haja ya Serikali na Sekta binafsi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha maendeleo yanaendelea kupatikana huku akiwataka watanzania kutumia falsafa na maono ya Mwl Nyerere kujipatia Maendeleo kwa mtu mmoja mmoja

“Ni vema kujiuliza Mwalimu Nyerere alikuwa ni mtu wa namna gani, alisimamia mambo gani na namna tunavyoweza kunufaika na
maono yake katika juhudi za kujiletea maendeleo,” alisema Dkt.Biteko na kuongeza kuwa ifahamike Mwalimu Nyerere alikuwa kijana mchapakazi, mwanafunzi shupavu, mpigania uhuru aliyetamani wakati wote haki, usawa, umoja, utu na maendeleo ya watu kwa watanzania.

Amesema baba wa Taifa katika uongozi wake alihakikisha ukuaji wa uchumi, siasa na kwamba hakuna nyanja ambayo hajawahi kuifanyia kazi hivyo Kongamano hili linalenga kuyaenzi mema yote aliyoyatenda

Pia aliamini elimu, uwekezaji na amani ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya watu

Biteko amesems Mwalimu Nyerere ni msingi wa ukombozi na maendeleo ya taifa na kwenye sera ya elimu ya kujitegemea alisisitiza elimu ni chombo cha kuleta usawa, ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi.

“Natamani kuona elimu inampa mwanafunzi maarifa ya kumuwezesha kuchangia maendeleo ya jamii yake na sio kujitenga na jamii yake,”alisema Biteko na kuongeza kuwa anatamani kuona wasomi baada ya kutoka vyuoni, wanachangia na kutatua changamoto za Jamii.

“Tujiulize elimu yetu inamjenga Mtanzania kujitegemea, dunia ya sasa yenye ushindani wa kiteknolojia na uchumi, ni muhimu sana elimu yetu kujibu changamoto za kijamii, tupunguze kuamini kwamba kuna watu watakuja kutatua changamoto zetu badala ya sisi wenyewe,” alisisitiza

Aidha amesema Mwalimu Nyerere alipinga maisha ya matabaka na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya watanzania wote na si kwa ajili ya kikundi cha watu wachache jambo ambalo hata sasa Serikali ya awamu ya sita imeendelea kulifanya

” Hayati Baba wa Taifa alipinga mifumo ya uchumi inayoleta matabaka na kuhimiza ujamaa na kujitegemea kwa kuamini taifa lenye usawa na watu wenye kupendana, kuheshimiana na kuhimiza utu na kazi linaleta amani na umoja,” alisema Dkt Biteko

Ameongeza kuwa tunapaswa kuwekeza fikra hizo kwa kuwekeza katika elimu, kilimo, viwanda, teknolojia, na biashara ambayo.inategemewa sana na watu wengi kujiinua kiuchumi.

Amesema Serikali na sekta binafsi zinapaswa kuhakikisha uwekezaji huo unaleta tija kwa wananchi na kuwaondolea umasikini walionao kwa kuzingatia kuwa
hakuna maendeleo yanayowezekana bila mshikamano wa kitaifa, usawa na maadili kwa watu wote

Pia amesema hayati alipinga ukabila na udini alipanda mbegu hiyo ambayo mataifa mengi wanatamani kuwa nayo kwa kuwa na mtazamo wa kuishi kwa umoja bila kujali dini zao, imani zao na makabila yao hali zao za kiuchumi na matabaka

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo hicho na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Tanzania Bara Stephen Wasira amewaasa baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuvuruga amani
kutambua kuwa amani ya nchi hii imejengwa katika mwamba na kwamba haiwezi kuvurugwa na mtu yeyote

Naye Mkuu wa Chuo hicho Prof Haruni Mapesa amesema Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kimekuwa na uraratibu wa kuandaa makongamano ya aina hi kila mwaka lengo likiwa ni kuwakutanisha wadau mbali mbali kwa pamoja kujadili Falsafa na maoni ya Muasisi wa Chuo Hayati Julius Kambarage Nyerere

Amesema makongamano hayo yanekuwa yakiendana na mada mbalimbali ambapo kwa mwaka huu mada Kuu ni Maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika Elimu, Uwekezaji na Ujenzi wa Taifa lenye Amani kwa Maendeleo ya Watu