May 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Biteko ataja mafanikio ya programu jumuishi ya malezi 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza 

Serikali imesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa na kutekeleza programu jumuishi ya taifa ya  malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ya mwaka 2021/22-2026, yenye lengo la  kuimarisha malezi ya watoto chini ya umri wa miaka 8.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko,wakati maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia na kongamano la malezi lililofanyika jijini Mwanza,lenye lengo la  kuthamini nafasi ya familia katika makuzi na malezi ya mtoto, ambao ndio msingi wa jamii bora.

Dkt.Biteko, amesema programu hiyo inahakikisha watoto wanapata huduma stahiki jumuishi za malezi kwa uwiano ulio sawa,kuanzia mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake hadi anapofikisha umri wa miaka 8.

“Kauli mbiu ya mwaka huu  inasema,’Mtoto ni malezi, msingi wa familia bora kwa taifa imara’,kauli hii inatukumbusha umuhimu wa kuzingatia malezi bora ya mtoto tangu akiwa tumboni hadi anapofikisha miaka 18,”.

Amesema,yapo mafanikio kadhaa yaliopatikana katika miaka mitatu ya utekelezaji wa programu hiyo ikiwemo kuwajengea uwezo walimu wa elimu ya awali 12,000 kutoka Halmashauri 184,  kutoa elimu ya malezi chanya ya watoto wakihudumia watoto zaidi ya watoto 360,000 nchini,kujenga vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 4,178  ambavyo vinatoa huduma ya malezi ya awali kwa watoto zaidi ya 400,000.

Pia vituo 206 vinavyomilikiwa na jamii,vvimekuwa  vikitoa huduma kwa watoto 11,675 na kuimarisha huduma za malezi kwa watoto wa miaka 5 hadi 8, serikali imejenga madarasa mapya ya elimu ya awali 1316 na kuwapatia vifaa vya kujifunza na kufundishia.

Huku kaya zaidi ya 15,000,zimefikiwa na elimu ya malezi jumuishi na huduma za afya ya jamii,ambapo imetolewa huduma ya afya bora,lishe,malezi,kupitia hisia za mtoto,elimu ya awali,kuchangamsha mtoto,ulinzi na usalama wa mtoto.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine,imetoa mafunzo kwa wataalamu zaidi ya 15,000, wakiwemo walezi wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana,hizo zote ni hatua ambazo tumefanikiwa kuzifikia.Ili tuendelee kufanikiwa ipo haja ya kuendelea kukumbushana wajibu na jukumu la kila mtu la malezi katika familia,”.

Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mwanaidi  khamis, amesema kuwa malezi ya mtoto yanaanza pindi anapokuwa tumboni, hivyo ni jukumu la pamoja la baba na mama kushirikiana katika malezi ili kuhakikisha watoto wanalelewa vizuri na kupata haki zao zote za msingi.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha utekelezaji wa programu ya malezi bora kwa watoto inasimamiwa kikamilifu na kwa mafanikio.