Fresha Kinasa TimesMajira Online Mara.
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko amewaongoza waombolezaji wakiwemo Viongozi wa serikali, Dini, Vyama, Mashirika pamoja na Wananchi kwa ujumla katika mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Boniface Gissima Nyamo-hanga.
Mhandisi Nyamo-hanga alifariki Dunia kwa ajali ya gari yeye na dereva wake Muhajiri Mohammed Haule usiku wa kuamkia Aprili 13, 2025,Wilayani Bunda Mkoani Mara.
Ambapo mazishi yake,yamefanyika Aprili 16, 2025,maeneo ya Migungani Wilayani Bunda huku huzuni, majonzi na vilio vikitanda kutoka kwa Waombolezaji waliofurika wakimlilia Mhandisi Gissima kutokana na uchapakazi wake, unyenyekevu, uhodari na uwajibikaji wake ulioleta mageuzi chanya.
Akizungumza wakati wa Hotuba yake ambayo wakati mwingine aliikatisha kwa muda kutokana na kutokwa machozi ya huzuni, Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko amesema Mhandisi Nyamo-hanga ameiongoza TANESCO kwa viwango vya juu na kwa kuijenga kuwa Taasisi imara na pia wakati mwingine alibeba lawama Kwa niaba ya watumishi wengine kutokana na unyenyekevu wake ili mambo yafanyike kwa ufanisi.

Ameongeza kuwa,Wizara hiyo itaendelea kumuenzi kwa mema yote aliyoyafanya katika sekta yake kwani alikuwa ni hazina kuu katika Mipango yenye mafanikio ikiwemo kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika na jambo hilo amelifanya kwa ufanisi. Huku pia akisema kabla ya kufikwa na mauti ameongoza mazungumzo na nchi ya Zambia hivi karibuni yenye tija ambapo wataanza kuiuzia umeme.
Aidha, Dkt. Biteko amewahakikishia Watanzania kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesikitishwa na kifo chake na alielekeza azikwe kwa heshima zote huku akibainisha kwamba Rais Dkt.Samia Hassan analojicho zuri la kuona hivyo Watanzania Waamini atachagua kiongozi bora na mahiri wa kuliongoza Shirika hilo kama Mhandisi Nyamo-hanga.
Pia, ameitaka familia iliyoachwa kuendelea kushikamana kwa upendo na kutokubali kugawanyika kipindi hiki ambacho Baba yao ameondoka na huku akisema Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika kipindi hiki kigumu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amewataka watumiaji wa barabara kuzingatia sheria wanapotumia barabara hizo. Huku akilitaka Jeshi la Polisi Mkoani humo kuongeza oparesheni kudhibiti ajali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu.
Naye Christopher Gachuma akizungumza Kwa niaba ya Familia ya Mhandisi Nyamo-hanga amesema, familia hiyo na Taifa wamepoteza mtu muhimu sana ambaye pia ni kiongozi ambaye alikuwa bado anahitajika kutokana na uchapakazi wake ambao ulikuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo.

Akihubiri katika ibada ya mazishi ya Mhandisi Nyamo-hanga Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT Dayosisi Mkoani Mara John Maguge Mwita amewakumbusha watu kuendelea kuishi maisha ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na kujitayarisha wakati wote kwani kifo huja ghafla.
“Kifo hakichagui wala kuangalia uwezo wa mtu am cheo chake, maskini hufa, matajiri hufa, wakubwa na wadogo pia. Niwaombe kujiweka tayari na kujiandaa. Tutambue kuwa haya ni mapenzi ya Mungu kumchukua mpendwa wake. Familia ishikamane na kumtegemea Mungu iache mawazo ambayo yanaweza kuwagawa wampe Mungu nafasi atawale maisha yetu.”amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TANESCO Dkt. Rhimo Nyansaho amesema miongoni mwa mambo ambayo atakumbukwa Mhandisi Nyamo-hanga ni mageuzi makubwa aliyoyafanya kufikisha Umeme Vijijini wakati akifanya kazi REA, kuleta mageuzi chanya TANESCO na kufanya kazi kwa weledi kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata Nishati kwa ajili ya maendeleo.
“Tunapopata vyeo tuwainue wafanyakazi wetu kwa kazi zao wanazozifanya, Mhandisi Nyamo-hanga alikuwa na moyo huo wa kuinua wengine. Jambo hili ni zuri Sana, tunapokuwa tunafanya kazi katika Ofisi tunalojukumu la kufanya hivyo kuwainua wenzetu, mwenzetu alifanya hivyo na ndio maana leo tumefurika kwa wingi kumpumuzisha mwenzetu.”amesema Dkt. Nyansaho.

HISTORIA YAKE.
Akisoma Wasifu wa marehemu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano TANESCO Makao Makuu Irine Gowele amesema kuwa, Mhandisi Boniface Gissima Nyamohanga alizaliwa Septemba 10, 1969 Mkoani Mara, akiwa mtoto wa tisa katika familia ya watoto 11. Ambapo alianza safari yake ya elimu katika shule ya Msingi Mlimani Jijini Dar esl laam na kuhitimu mwaka 1984. Aliendelea na masomo ya Sekondari katika shule ya Azania 1985-1988 na kisha kidato cha Tano na Sita katika shule ya Sekondari Kibaha akihitimu mwaka 1991.
Gowele amesema, Mwaka 1992 alijiunga na Chuo kikuu cha Dar es laam na kuhitimu shahada ya Uhandisi wa umeme. Baadaye alijipatia Shahada ya Uzamili ya usimamizi wa Uhandisi (2009-2011) na Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara (MBA) (2012-2014) zote kutoka Chuo Kikuu hicho hicho.
Aidha, wakati huo huo alihitimu pia Stashahada ya juu ya sheria za uamzi na usuluhishi katika rasilimali watu kutoka Chuo Cha Ustawi wa Jamii. Mwaka 2014, alijiunga na Chuo Kikuu Cha Strathclyde nchini Scotland na kuhitimu shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Fedha mwaka 2018.
Pia amesema, Mwaka 1996 hadi 2004 Mhandisi Nyamo-hanga alianza kazi katika Kampuni ya BP Tanzania kama Msaidizi wa mauzo ya Solar na kupanda vyeo Hadi nafasi ya Uhandisi akijikita katika Nishati mbadala. Na mwaka 2004 hadi 2008 alijiunga na Kampuni ya Business Care Services na Esd Limited Uingereza akihudumu kama Mshauri wa Nishati na Maliasili akitoa ushauri wa Kitaalamu katika masuala ya Nishati endelevu.
Mhandisi Nyamo-hanga aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO tarehe 22 Septemba 2023 hadi kufariki kwake tarehe 13 Aprili 2025.


More Stories
Chalamila:Dar ni salama,aelezea mafanikio na mipango ya maendeleo ya Mkoa
Ulaji vyakula vya aina moja,umri vyatajwa ongozeko la matatizo ya macho Mbeya
Kenya,Uganda zaanzisha mradi wa uendelezaji rasilimali za maji Angololo