Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Imeelezwa kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),imesimamia utekelezaji wa masuala ya ajira kwa wazawa hususani katika miradi mikubwa ya sekta ya nishati ikiwemo mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Hayo yamebainishwa Machi 24,2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt. Doto Biteko,wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,walioitaka Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania wanapewa kipaumbele cha ajira katika miradi ya kimkakati ya sekta ya nishati.

Dkt.Biteko ameeleza kuwa, EWURA imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha sera na miongozo ya ushiriki wa wazawa inatekelezwa kwa ufanisi, jambo ambalo limewezesha wazawa kunufaika na fursa za ajira na zabuni katika miradi mikubwa.
“EWURA imefanya kazi kubwa kuhakikisha watanzania wananufaika na fursa zilizopo katika miradi ya kimkakati kama EACOP. Naipongeza kwa kazi hii inayoendelea kufanya. Niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kusimamia sera za ushiriki wa wazawa ili kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wake,”amesema Dkt. Biteko.
Pia asisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati ili kuimarisha ushiriki wa wazawa katika miradi yote inayoendelea na inayotarajiwa kuanza kutekelezwa nchini.

More Stories
Tanzania yaadhimisha siku ya hali ya hewa,kwa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma zake.
Samamba:Uongezaji thamani madini ni mkakati wa serikali kukuza mchango wa sekta
Prof.Muhongo apongezwa kuleta majadiliano sekta ya elimu Musoma