Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula kwa kushirikiana na wananchi wa mtaa wa Mhonze wamejenga vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja katika shule ya msingi Umoja iliopo Kata ya Shibula jimboni humo huku kiasi cha milioni 35 kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
Ujenzi huo ambao umefikia hatua ya boma kupitia mchango wa wananchi huku Mbunge Dkt.Angeline amechangia tofali 3,500,lengo likiwa ni kupunguza mrundikano wa wanafunzi darasani katika shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 900 huku madarasa yakiwa 6.
Hayo yamebainishwa Julai 18,2024 katika ziara ya Mbunge huyo baada ya kutembelea shule hiyo kwa ajili ya kujionea utekelezaji wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa kupitia kauli mbiu ya “Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga”,ikiwa na maana ya kuwa wananchi wanaanzisha msingi,Mbunge anatoa tofali za kujenga boma na Halmashauri inamalizia.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Umoja Zacharia Majigwa, ameeleza kuwa Mbunge na wananchi baada ya kuona adha wanayoipata wanafunzi wa shule hiyo wakaanzisha ujenzi wa madarasa hayo ili kuweka mazingira bora ya kujifunza na kufundishia.
“Shule ina wanafunzi 996 wa darasa la kwanza hadi la saba ambao wanatumia vyumba 6 vya madarasa lakini darasa la awali wapo wanafunzi 78 ambao tumewaazimia darasa kwa shule mama ya jirani ya Mhonze,nitashukuru kilio chetu kikisikiwa kwa ajili ya kukamilishiwa kwa wakati vyumba hivi vitatu na ofisi moja,”ameeleza Mwl.Majigwa na kuongeza kuwa;
“Kwa namna moja watakuwa wametusaidia kupunguza hii adha ya msongamano darasani, kwa darasa la kwanza pekee yake lina wanafunzi 141, kwa chumba kimoja na hicho hicho chumba kinatumika kwa wanafunzi wa darasa la pili ambao wapo 168, wanapishana hawa wanaingia asubuhi wanatoka saa tano na la pili wanaingia na kutoka saa nane mchana,”.
Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya msingi Umoja Elias,amesema madarasa matatu na ofisi moja yamejengwa kwa nguvu za wananchi ambapo kila darasa lilichangiwa na mtaa kiasi cha milioni 3,610,000 pamoja na mchango wa Mbunge.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula, ameeleza kuwa ukiangalia hali halisi ya msongamano ata kiafya siyo nzuri ambapo shule hiyo imeisha tengewa kiasi cha milioni 35 katika bajeti ambayo imeanza mwezi huu wa Julai.
“Tuna utaratibu wetu wa ‘Ilemela ni yetu tushirikiane kuijenga,’kwaio mwananchi anapoweka nguvu yake , Mbunge anachangia na baadae Halmashauri inasaidia,”ameeleza Dkt.Angeline.
Sanjari na hayo ameeleza Kata ya Shibula imepatiwa kiasi cha zaidi ya milioni 900 na serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya ya msingi na sekondari.
“Katika fedha hizo milioni 584 inaenda kujenga shule mpya ya sekondari Masemele na zile milioni 300 na, nazo zimekuja kwa ajili ya shule ya msingi ambayo ijengwe eneo jingine ambalo halina migogoro na watoto wanatembea umbali mrefu kufuata elimu na siyo Masemele ambapo tayari shule ya msingi ipo,”.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Kata ya Shibula Amosi Lugisa ameeleza kuwa kama chama wameshauri shule ya msingi mpya ikajengwe mtaa wa Semba’A’ eneo lipo na wananchi wapo tayari kulilipia.
“Ambapo mitaa ya Semba’A’ na Semba’B’ haina shule ya msingi watoto wanatembea umbali mrefu kuja kwenye shule ya Mhonze au Umoja na katikati kunajengwa barabara ya lami na vijana wetu kwa sababu ni wageni wa barabara ya lami wanaweza kupata ajali,eneo lipo tayari na wananchi wameisha kubaliana kuwa watalilipa wanapo enda kulipia viwanja vyao wanakata fedha fulani kwa ajili ya kulipia maeneo kama haya ya matumizi ya umma,”.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato