November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Angeline: Rais Samia apongezwe kwa kuweka usawa wa kijinsia

Judith Ferdinand, Mwanza

Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,amesema jamii haiwezi kuwa na kizazi chenye usawa kama hakuna chombo kinachosimamia suala hilo.

Kwani kumekuwa na majukwaa mbalimbali ya kupigania usawa lakini yameshindwa kufikia malengo.

Hivyo kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan cha kukusudia kutenganisha Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii kuwa wizara mbili tofauti ni cha kuungwa mkono na kupongezwa kwani kitaongeza kasi ya usimamizi wa masuala hayo.

Dkt.Angeline amesema hayo wakati wa hafla la wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali kwa mabinti waliokosa elimu katika mfumo rasmi yaliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Zawadi Yangu Initiative iliyoko Kata ya Mecco wilayano Ilemela mkoani Mwanza.

Amesema,kutenganisha kwa wizara hiyo ni jambo linaloenda kuweka mabadiliko chanya,wataenda kuona kasi ya maendeleo kwa kugusa jinsia zote katika utendaji.

Pia itasaidia kufikia lengo la kuwepo kwa usawa wa kijinsia na kuwakomboa wanawake kiuchumi.

“Tunapozungumzia masuala ya uwezeshaji kiuchumi na kuleta usawa wa kijinsia maanake sasa tutakuwa tumeyagusa makundi yote lakini anaelengwa zaidi ni mwanamke ambaye kidogo amekuwa nyuma katika mambo mengi,tumshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia, haki na ukombozi wa kiuchumi kwa jinsia zote,”amesema Dkt.Angeline.

Pia amesema,serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kumkomboa mwanamke ikiwemo kuendelea kutoa elimu bila malipo,fursa kwa mabinti watakaopata ujauzito kwa bahati mbaya kuendelea na shule kama sheria na sera itakavyoelekeza pamoja na kufuta tozo zaidi ya 108 zilizokuwa kero katika masuala ya umiliki wa ardhi na nyanja nyenginezo.

Mratibu wa mradi huo wa shirika la Zawadi Yangu Initiative Attupele Mwakitalu, amesema shirika hilo limejikita katika kuwezesha wanawake na wasichana pamoja na kulinda na kutetea haki za watoto hasa wa kike na zaidi kuwawezesha wanawake kujikwamua dhidi ya adui maskini na kuwa na familia imara zenye afya njema.

Mwakitalu amesema,pia linatoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake ili kuinua viwango vya ujuzi na kuwapatia fursa za kujiajiri na kuajiriwa.

Amesema wamepata mafanikio kwani kuanzia Agousti 2017 darasa la kwanza la ushonaji lilianza likiwa na wanafunzi 26,kundi la pili mwaka 2018 wanafunzi 25,kundi la tatu mwaka 2019wanafunzi 35 ,kundi la nne mwaka 2020 wanafunzi 46 huku kundi la tano ndio hilo la mwaka 2021 wanafunzi walikuwa 56 ila waliohitimu ni 44 bahati mbaya 12 waliacha mafunzo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba,umbali kutoka makazi wanayoishi na kuhama.

“Tangu kuanzisha kwa mafunzo hayo Zawadi Yangu Initiative imeisha toa mafunzo hayo ambayo ni bure 176, tunajisikia fahari sana kwani tumekuwa sehemu ya mchango katika taifa letu la kuinua wanawake na vijana wa kike na ushonaji ni ajira kama ajira nyingine,” amesema Mwakitalu.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi ambaye ni Dkt.Angeline, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo Grace Jeremiah,ameishukuru taasisi ya Zawadi Initiative kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwani yatawasaidia katika kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira pamoja na kuleta ushindani katika soko.

Pia ametoa ombi kwa mgeni rasmi la kusaidiwa kupata mkopo wa wanawake na vijana unaotolewa na Halmashauri ili uwasaidie katika kuendeleza ujuzi wao kama kikundi cha wajasiriamali wa Zawadi Yangu Initiative 2021.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Sitta Singibala, amewahimiza wahitimu hao kufanyia kazi elimu walioipata na ili waweze kupata mtaji kwa ajili ya kufanyia shughuli zao kutokana na ujuzi walioupata wajiunge katika vikundi ili waweze kupata mkopo kutoka halmashauri ambao hauna riba na kuweza kujikwamua kiuchumi.

Diwani wa Kata ya Buzuruga Manusura Sadick,amewahakikishia ushirikiano katika kuhakikisha wanakuwa na mazingira rafiki ya kujiajiri na kujiletea maendeleo.

Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula akizungumza wakati wa hafla la wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali kwa mabinti waliokosa elimu katika mfumo rasmi yaliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Zawadi Yangu Initiative iliyoko Kata ya Mecco wilayano Ilemela mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya ushonaji katika hafla ya wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali kwa mabinti waliokosa elimu katika mfumo rasmi yaliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Zawadi Yangu Initiative iliyoko Kata ya Mecco wilayano Ilemela mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya ushonaji katika hafla la wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali kwa mabinti waliokosa elimu katika mfumo rasmi yaliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Zawadi Yangu Initiative iliyoko Kata ya Mecco wilayano Ilemela mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand