Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ametoa mwezi mmoja kwa Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mwanza kuhakikisha anashughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi ya namna zoezi la utoaji hati linavyoendeshwa kwa kusuasua na kuchukua muda mrefu tofauti na inavyoelekezwa.
Agizo hilo amelitoa alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi ya Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kufuatilia maduhuri ya Serikali pamoja na kukagua utendaji kazi wa makampuni binafsi yanayoendesha zoezi la urasimishaji wa makazi, umilikishaji na utoaji hati miliki kwa wananchi.
Amesema kuwa, wananchi wamekuwa wakilalamikia namna zoezi la utoaji hati linavyoendeshwa kwa kusuasua na kuchukua muda mrefu tofauti na inavyoelekezwa sanjari na kutoridhishwa na kazi ya urasimishaji makazi iliyokaimishwa kwa makampuni binafsi ya upimaji kwani yamekuwa yakikusanya fedha za wananchi huku kasi ya upimaji na umilikishwaji ikiwa ndogo ukilinganisha na mwitikio wa wananchi jambo lililomfanya kutoa mwezi mmoja kwa Kamishina Msaidizi huyo wa ardhi hahakikishe anashughulikia kero hizo.
“Nakupa mwezi mmoja uwe umeshughulikia kero hizo kwani lengo la Serikali ni kukusanya kodi msipowamilikisha tunakusanyaje hiyo kodi,lakini wananchi wanachanga fedha zao halafu makampuni hayatoi huduma, naelekeza kampuni zote zilizochukua fedha za wananchi na hakuna kilichofanyika yapelekwe kwenye vyombo vya sheria,” amesema Dkt.Angeline.
Pia amekemea makusanyo hafifu ya kodi ya ardhi ambapo kwa mujibu wa bajeti kiasi cha bilioni 2 kinategemewa kukusanywa kwa Mkoa wa Mwanza lakini mpaka sasa jumla ya milioni 50 pekee ndio iliyokusanywa kutokana na mwitikio hafifu wa wananchi wakati serikali imetoa milioni 30 kwaajili ya kuendesha vipindi vya redio na luninga vya uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa wananchi.
Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mwanza Biswalo Makwasa aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri huyo huku akisema ziara hiyo imesaidia kuboresha utendaji wao wa kazi sanjari na kuongeza kuwa kuwa mpaka sasa Ilani 10,000(notice) za kuwakumbusha watu kulipa kodi hizo zimekwisha sambazwa kwa wadaiwa hivyo maagizo yamekuja wakati muafaka na yamewaongezea kasi ya utendaji kazi.
Naye Msajili Msaidizi wa Hati Mkoa wa Mwanza Ivan Amurike amesema changamoto zinazochangia kupunguza kasi ya utoaji hati na ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali ikiwemo kutojitokeza kwa wamiliki wa ardhi kuchukua hati miliki pindi zinapokamilika.
More Stories
CPA.Makalla :CCM kutumia 4R za Rais Samia katika uchaguzi Serikali za Mitaa
CCM kutumia 4R za Samia Uchaguzi Serikali za Mitaa
Dkt. Mpango awasilisha salam za Rais Samia mazisha Baba yake mzazi, Gavana Tutuba