Na Judith Ferdinand, TimesMajira, Mwanza
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza kimezindua rasmi kampeni zake huku Mgombe Ubunge Jimbo hilo Dkt. Angeline Mabula akiwaomba wananchi wamtume tena kwa miaka mingine mitano ili aweze kumalizia kazi na kuibua mambo mengine ya kimaendeleo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo uliofanyika katika uwanja wa Sabasaba kata ya Ilemela, Dkt. Mabula amesema, kwa kipindi cha miaka mitano wamefanikiwa kutatua migogoro ya ardhi, kutoa mikopo ya kinamama, vijana na walemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri, kujenga na kuboresha miundombinu ikiwemo shule, barabara pamoja na usafiri katika kivuko cha Bezi na Kayenze.
Kulingana na kuboresha miundombinu katika sekta ya uvuvi pale walipokuwa wanakusanya mapato ya Sh. milioni 30 yameongezeka na sasa wanakusanya zaidi ya Sh. milioni 100 ambapo changamoto zilizobaki ni za kupapasa hivyo amewaomba tena wamchague ili akamalizie.
“Wananchi mnamtambua wazi mlipotoka, mlipo lakini mnapoelekea hampajui hivyo mkikiamini Chama cha Mapinduzi na mtambue kina dhamira ya dhati kuhakikisha Taifa linasonga mbele huku mwelekeo wetu ukiwa ni chanya katika kuijenga Tanzania mpya,usiniunue betri mpya ambapo katika betri zako katikati ukaweka guzi hapo tochi haitawaka hivyo nawaomba mnitume ,niwatumikie kwa sababu mie ni kiungo mshambuliaji nitakaye waletea maendeleo,”amesema Dkt. Angeline.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela Nelson Mesha, amewashukuru wananchi kwa kukiamini chama hicho na kuwachagua viongozi kutoka chama hicho mwaka 2015 na kuweza kuwasaidia kutafsiri ilani ya chama hicho katika mambo mbalimbali ikiwemo kuchangia ujenzi wa madarasa.
“Naomba wananchi mtuunge tena mkono ili mbunge aweze kumalizia kazi iliobaki na siku ya kupiga kura mtupigie mafiga matatu yani Rais,Mbunge na Madiwani wa kata zote 19 zilizopo jimboni humu ili nao wamalizie kazi,” amesema Mesha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James ambaye alikua mgeni rasmi katika uzinduzi huo alisema,kazi waliotumwa kwa miaka mitano wameifanya.
“Mwaka 2015 wakati tunakuja kuomba kura hapa barabara hii ya Sabasaba -Kiseke -Buswelu ilikuwa mbovu na watu walikuwa wanalalamika lakini sasa imejengwa na inapitika,kulikuwa hakuna hospitali ya Wilaya Ilemela lakini sasa tayari imejengwa pia katika kipindi cha miaka mitano mambo mengi yamefanyika ikiwemo hospitali, shule,reli,meli,ndege na vitu vingine hivyo nawashangaa wanaosema kuwa tumeleta maendeleo ya vitu wakati vitu haviwezi kutumia vitu hivyo na wanao nufaika ni watu,” amesema James
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi