May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dk. Mpango aipongeza NMB kampeni ya Upandaji Miti, Shule zatengewa Mil. 472/-

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango, ameipongeza Benki ya NMB na kuitaja kuwa kinara katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kupambana na Athari za Mabadiliko ya tabianchi.

Dk. Mpango Ametoa pongezi hizo baada ya NMB kuzindua Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti Milioni 1 kwa kushirikiana na Wakala huduma za Misitu Tanzania (TFS), huku ikitenga kiasi cha Sh. Milioni 472 kuzizawadia shule zitakazofanya vema katika shindano la utunzaji na uhifadhi wa miti.

Uzinduzi huo sambamba na upandaji wa miti 3,000 ya matunda, kivuli, mbao na dawa, umefanyika katika Mji wa Serikali,  Mtumba, jijini Dodoma, hafla iliyohudhuriwa na mawaziri, viongozi mbalimbali wa Serikali, Wadau wa Mazingira, wanafunzi wa shule na Vyuo Vikuu, watumishi wa benki ya NMB wakiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB,  Ruth Zaipuna na Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Dk. Edwin Mhede.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mpango amesema kampeni hiyo chanya inaitia moyo ofisi yake, na kubainisha kuwa kutokana na ukweli kwamba bila miti hakuna mvua, chakula, maji, hewa safi na ndio chanzo cha mafuriko na athari nyingine za Mabadiliko ya Tabianchi, Serikali inahitaji uungwaji mkono kama unaofanywa na NMB.

“kinachofanywa leo na NMB ni cha kuigwa na kupongezwa, kampeni hii inaenda kusapoti pakubwa jitihada za Rais Samia, ambaye amejipambanua katika hili, amekuwa kiongozi mwenye mkazo wa suala la mazingira tangu akiwa waziri, kisha Makamu wa Rais na sasa akiwa Rais wa Tanzania, akitambua kuwa mazingira yanagusa sekta zote kimaendeleo.

“Na kwa mantiki hiyo, nasisitiza kuomba wadau wa mazingira, mashirika, kampuni, taasisi na jamii kwa ujumla, kujitoa katika kumsapoti Rais Samia, kwani Serikali Pekee haiwezi kufanikisha mapambano haya.

Ndio maana naipongeza NMB kwa uharaka wao kuitikia wito huo, zaidi kwa kuongeza fungu la Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), sambamba na kubuni shindano la upandaji miti, utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwenye shule zetu.

“Kuna maana kubwa kwa NMB kuongeza Shilingi Bilioni 2 kwenye CSR, ambazo ni maalum kwa ajili ya mazingira, lakini kama haitoshi Ikatenga Sh. Milioni  472 kuzizawadia shule zitakazofanya vema katika shindano la upandaji na utunzaji miti linalozinduliwa sanjari na kampeni hii.

Zawadi za shule washindi ni nono na kutokana na uwingi wake na idadi ya wanafunzi,  maana yake elimu inaenda kuifikia jamii kirahisi,” alifafanua Dk. Mpango.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisisitiza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi hazijawahi kumuacha yeyote

salama na kwa kutambua hilo, benki yake ikaongeza fungu lake la CSR kutoka Sh. Bilioni 4.2 (ambazo ni asilimia 1 ya faida yao kwa mwaka Sh. Bil. 429), hadi kufikia Sh. Bilioni 6.2, ongezeko linalothibitisha namna wanavyojali na kuthamini mazingira.

Aidha, akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Suleiman Jafo alisema kuwa wizara yake iko tayari kushirikiana vyema na Benki ya NMB na kuhakikisha kuwa adhma ya kupanda miti milioni moja kwa mwaka 2023 inatimia kikamilifu.

“Wizara yetu haitahakikisha miti hii milioni imepandwa lakini tutahakikisha miti hii yote inkuwa na kustahimili ili iweze kuleta tija katika mazingira yetu na kuwa na manufaa kwetu,” alisema Mhe. Dkt. Jafo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali na Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angella Kairuki alimuhakikishia Makamu wa Rais kuwa wizara ya TAMISEMI watahakikisha uratibu wa mashule katika shindano lililoasisiwa na Benki ya NMB unaenda kiufasaha na shule nyingi katika hlamashauri zote nchini zitashiriki.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Edwin Mhede alisema kuwa Benki ya NMB imeamua kuja na kampeni hii kwani ni Ajenda ya kidunia na taasis kama NMB hawana Budi kuja na kampeni kama hii kwani ni jambo lenye manufaa kwa taifa.

Katika hafla hiyo, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo alisema kuwa wata hakikisha wana shirikiana vyema na Benki ya NMB kwa kuwapatia mishe bora ya miti pamoja na utaalamu walionao katika masuala ya miti ili kuhakikisha kampeni ya miti milioni inatimia.