Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
DIWANI wa Viti Maalum Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mkoa wa Dar es Salaam, Hawa Abdulrahman, amewatembelea wanafunzi wa shule zote kata ya Manzese na kuwataka kuwa watulivu katika kipindi hiki kutokana na taharuki ya utekaji wa watoto
Kauli hiyo ametoa leo Julai 24, 2024 alipokuwa akizungumza na wazazi, walezi na walimu katika shule za Ukombozi, Kilimani, Uzuri, pamoja na Shule ya Sekondari Manzese ambapo hivi karibuni kumetokea taharuki katika maeneo mbalimbali.
“Sisi kama wazazi tunajukumu la kuwalinda watoto na pia kuhakikisha mnapata elimu bila vikwazo vyovyote,” amesema Hawa.
Naye mtedaji wa kata hiyo, Rozina Kimario, amesisitiza mahudhurio katika shule zote na atahakikisha anafuatilia kwa karibu hususani kipindi hiki cha taharuki.
“Kama Serikali tuna jukumu la kuhakikisha usalama wa mtoto kwa kipindi chote akiwa shule, lakini pia wazazi wenye tabia ya kuwaacha watoto na kuwa wakaidi kwenda shule bila sababu ya msingi tutaendelea kuwachukulia hatua. Shule tunajua mtoto anaumwa, mzazi naye anajua mtoto yupo shule kumbe mtoto yupo mitaani na vijiweni.
“Naomba wazazi wenzangu tusaidiane mawasiliano ya karibu katika kuhakikisha watoto wetu wanapata haki zao za msingi kama elimu bila ubabaishaji,” amesema.
Katika ziara hiyo Diwani Hawa, aliambatana na viongozi wa Jumuiya za CCM za UWT, Wazazi pamoja na wenyeviti wa Serikali za Mitaa ya Chakula Bora na Kilimani.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato