Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, Tunduma.
SERIKALI ya Zambia imeyaruhusu malori 31 yakiwa na tani 1000 za mahindi ya wafanyabiashara wa Tanzania yaliyozuiliwa katika mji wa mpakani wa Nakonde, ikiwa ni hatua ya awali ya kuruhusu malori yote 40 yaliyozuiliwa nchini humo kwa zaidi ya miezi sita baada ya serikali ya nchi hiyo kuzuia uuzaji wa mazao ya chakula nje ya nchi .
Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael, alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Kitanzania katika mpaka wa Tunduma ambapo kwa muda mrefu wafanyabiashara hao waliweka kambi mpakani hapo wakiendelea na jitihada mbalimbali za kukomboa shehena hiyo.
Mkuu wa Mkoa alisema
shehena hiyo ya mahindi iliyokuwa imekwama nchini Zambia, yameruhusiwa kuingizwa nchini baada ya Serikali ya Tanzania na Zambia kutatua changamoto hiyo kidipromasia kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili.
“Kitendo cha wenzetu wa Zambia kuruhusu malori haya 31yakiwa na tani 1999 ni hatua za awali za kuruhusu mahindi yote yaliyokwama nchini humo na hili limefanikishwa kufuatia mazungumzo ya pande mbili yaliyolenga kuimarisha uhusiano zaidi” alisema Dk. Michael.
Inadaiwa kuwa mahindi hayo yalinunuliwa na wafanyabiashara hao kwa kusudi la kuyaingiza nchini miezi sita iliyopita, kwa kuzingatia taratibu zote za nchi hiyo, lakini baadaye kutokana na nchi hiyo kuona inakabiliwa na upungufu wa chakula mwaka huu, ilifunga mpaka na hivyo kuzuia mazao ya nafaka kutoka nje.
Kwa upande wao wafanyabiashara hao waliipongeza serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kuingilia kati suala hilo, Keanu walikuwa katika hatari kubwa ya kupoteza mahindi hayo pamoja na fedha walizokopa katika taasisi za kifedha kwa ajili ya kununulia mzigo huo .
“Tunamshukuru sana Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) kwa kuwezesha mzigo wetu kuvuka, kwani tulishaanza kukata tamaa ya kupoteza kila kitu na sijui tungepata wapi fedha nyingine za kufanya marejesho ya mikopo tuliyokopa benki. alisema mmoja wa wafanyabiashara hao Absoloum Mbuto.
Mbuto alisema serikali ya Zambia ilizuia mahindi yao kwa takribani miezi 6 bila sababu za msingi huku wakiwa na nyaraka zote za ununuzi na usafirishaji.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu