Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WAKATI mashabiki wakisubiri kwa hamu kubwa kumpokea kocha wao mpya Cedric Kaze aliyesemakana angetua hapa chini mwishoni mwa wiki iliyipita, sasa ni wazi Yanga wameamua kuchana na kocha huyo ambaye ametoa udhuru na kudai kuchelewa kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaoanza kutimua vumbi Septemba 6.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano imeweka wazi kuwa Kaze aliyekuwa ajiunge na wachezaji siku yoyote kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao wa kirafiki katika maandhimisho ya Wiki ya Mwananchi, ametoa udhuru na kuomba kuchelewa kujiunga na timu kwa wiki tatu zaidi kutokana na matatizo ya kifamilia.
Kocha huyo ametuma ujumbe akiomba wiki tatu zaidi kutokana na matatizo hayo jambo lililowafanya uongozi kubadili haraka maamuzi yao na kutafuta kocha mwingine kutoka kwenye orodha ya waliokuwa wamepeleka maombi awali haraka iwezekanavyo.
Kutokana na sababu hiyo viongozi walifanya kikao cha dharura na kukubalina kutangaza kocha mwingine mpya atakayekuja kujiunga na timu hiyo haraka.
Kabla ya Yanga kutoa taarifa hiyo, taarifa ambazo hazikuwa rasmi zilidai kuwa, kocha huyo amegoma kujiunga na timu hiyo kurithi mikoba ya kocha Luc Eymael aliyetimuliwa mwishoni mwa msimu baada ya kusambaa kwa sauti yake akitoa maneno ya kibaguzi kwa mashabiki huku pia akitupa lawama kwa viongozi wa klabu hiyo pamoja na wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) .
Sababu za Yanga kuvutiwa na kocha huyo raia wa Burundi anayeishi Canada ni rekodi zake kwani ni miongizo mwa makocha wachache wenye leseni A za Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na Leseni ya Chama chama cha Soka cha ujerumani (DFB).
Tayari uongozi wa klabu hiyo ulishaanza maandalizi ya mapokezi na kuweka wazi kuwa, kocha huyo atatua hapa nchini na ataungana na wasaidizi ambao amewapendekeza kufanya nao kazi.
Kutokana na sifa za kocha huyo, mashabiki wa Yanga walisema watamtendea haki kwa kumpa mapokezi ya aina yake pengine hata zaidi ya yale waliyowapa wachezaji wao wapya, Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe siku chache zilizopita.
Miongoni mwa watu ambao inasemekana kocha huyo amewapendekeza ili kufanya nao kazi ni msaidizi wake pamoja na kocha wa makipa tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambapo uongozi ulikuwa ukiwatafuta.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship