January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DCPC FC mabingwa bonanza la DCPC, Polisi Temeke

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Onine

TIMU ya soka ya klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), imefanikiwa kunyakuwa ubingwa wa Bonanza la DCPC wakishirikiana na jeshi la Polisi mkoa wa Temeke, lililofanyika jana katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke.

DCPC ilinyakuwa ubingwa huo, baada ya kuwafunga Polisi Jamii kwa mikwaju ya penalti 4-3, katika mchezo wa fainali uliokuwa wa vute nikuvute kutokana na timu zote kuoneshana umwamba ndani ya dakika 90 na kutoka suluhu bila ya kufungana.

Hata hivyo timu ya DCPC FC, ilipongezwa na mashabiki mbalimbali waliohudhuria bonanza
hilo kutokana na kuonesha kiwango cha hali ya juu kwa kushindana na kikosi kinachofundishwa na aliyekuwa mchezaji wa Mtibwa Sugar na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Shabani Nditi.

Timu hiyo ya klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam, walingia hatua ya fainali baada ya kuichapa kombani ya Polisi mkoa wa Temeke goli 2-1, katika mchezo wa kwanza ulianza mapema.

Akizungumza kwa furaha nahodha wa DCPC FC, Alumanus Julius amesema aamini kama wangechukua kombe la bonanza hilo kwani walikutana na timu ngumu lakini wachezaji wenzake walipambana kuhakikisha wanalitwaa kombe hilo.

“Ki ukweli wacha niwe na furaha kwani hatukutegemea kukutana na timu zenye wachezaji wazuri ambao baadhi yao wanacheza ligi mbalimbali lakini nasi tulikuwa imara sana kufanikisha kile ambacho tunakihitaji,” amesena nahodha huyo.

Ametoa wito kwa timu hiyo, isiishie hapo bali iwe ya kudumu na kushiriki mabonanza mbalimbali ili kuitangaza timu ya waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke ACP. Kungu Malulu amewataka waandishi wa habari pamoja na Polisi wawe na mahusiano mazuri yenye kuleta tija katika kazi zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Samson Kamalamo ameipongeza timu DCPC FC kwa kuiheshimisha taaluma ya uandishi wa habari kupitia michezo.

Lakini, pia amelipongeza jeshi la Polisi kwa ushirikiano mzuri katika kuandaa bonaza hilo ambalo limeleta tija kubwa katika kada hizo mbili ambazo mara nyingi zimekuwa zikishirikiana katika utendaji wa kazi.

Lengo la bonanza hilo lilikuwa kujenga mahusiano mazuri baina ya waandishi wa habari na jeshi la Polisi nchini.