Na Agnes Alcardo, Timesmajiraonline. Dar
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Shirika la Posta Tanzania (TPC), zimetiliana saini hati ya ushirikiano, ikilenga kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya kupitia mtandao wa posta.
Makubaliano hayo yaliwekwa saini na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo na Postamasta Mkuu wa TPC, Macrice Mbodo, ikielezwa kuwa hatua muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.
DCEA imebainisha kuwa, wahalifu wamekuwa wakitumia mbinu za kusafirisha dawa za kulevya kupitia vifurushi na mizigo, huku kati ya dawa zilizokamatwa ni pamoja na mirungi (kilo 39,928.99), heroin (gramu 1,304.17), cocaine (gramu 673.55) na dawa tiba zenye asili ya kulevya kama morphine na codeine.
Ushirikiano huo utahusisha mafunzo ya watumishi, kuboresha vifaa vya utambuzi na kubadilishana taarifa kwa wakati ili kuimarisha ufanisi wa ukaguzi.
Postamasta Mkuu huyo, Mbodo amesisitiza kwamba, Shirika la Posta limejipanga kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa bidhaa kupitia mtandao wake, akirejea sheria na miongozo ya kitaifa na kimataifa, amesema mtandao wa Posta hautaruhusu bidhaa haramu kama dawa za kulevya, silaha, na nyara za serikali kupita bila kugundulika.
Teknolojia ya kisasa imerahisisha usafirishaji wa dawa mpya za kulevya kupitia mifumo ya kifedha ya kidijitali na majukwaa ya siri kama “dark web” hata hivyo, mtambo wa kisasa uliotolewa na DCEA umeimarisha uwezo wa TPC kubaini dawa hizo bila kufungua vifurushi, hatua ambayo Bw. Mbodo aliitaja kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto hizi.
Aidha Kamishna Jenerali Lyimo, amewashukuru wadau wote wanaoshiriki katika vita dhidi ya dawa za kulevya, akiwataka Watanzania kutoa taarifa za wahalifu na kushirikiana na serikali kuhakikisha mtandao wa posta unabaki salama. Alieleza kuwa ushirikiano huu unatoa ujumbe wa wazi kwa wahalifu kuwa vitendo vyao havitavumiliwa.
Makubaliano haya yamepongezwa kama juhudi za kuimarisha uchumi na kulinda jamii dhidi ya athari za dawa za kulevya. Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetajwa kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha taasisi kama DCEA na TPC kufanikisha mapambano haya.
More Stories
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba
Kliniki ya sheria bila malipo yazinduliwa Kilimanjaro