Na Jackline Martin, TimesMajira Online
BENKI ya Biashara ya DCB imepata faida kwa kiwango kikubwa kwa mwaka wa fedha wa 2022 ukilinganisha na faida iliyopatikana kwa kipindi kama hicho mwaka 2021, huku mali za benki hiyo na amana zikiongezeka.
Katika mwaka wa fedha wa 2022, benki ya DCB ilijipatia faida kabla ya kodi ya shilingi za Kitanzania 2.25 bilioni, ikilinganishwa na faida ya sh. 1.06 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021, ikiwa ni kukua kwa faida kwa asilimia 112.
Ukuaji huu unatokana na kuongezeka kwa mapato ya benki kwa asilimia 11, ambapo ulisababishwa na ukuaji wa mapato yatokanayo na riba ambayo yaliongezeka kwa asilimia nne hadi kufikia sh. 28.61 bilioni, ikilinganishwa na sh. 27.62 bilioni mwaka 2021, na mapato yasiyotokana na riba ambayo yaliongezeka kwa asilimia 45 kutoka sh. 7.2 bilioni hadi sh. bilioni 10.4 kati ya mwaka 2021 na 2022 kwa pamoja.
“ Benki ilifanikiwa kukuza mapato katika mwaka wa fedha ikijikita katika shughuli za utoaji wa mikopo kwenye shughuli za biashara, biashara ya fedha za kigeni, na ongezeko la ada ya miamala kutokana na maboresho ya vitengo mbalimbali vya huduma na ongezeko la matumizi ya huduma za kibenki kidigitali,” amesema Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa DCB , Siriaki Surumbu.
Benki vile vile iliimarisha nafasi yake kama benki ya ukubwa wa kati yenye mizania ya sh. bilioni 200, mali zake zikifikia thamani ya shilingi bilioni 214 kwa mwaka 2022.
“Huu ni ukuaji wa asilimia 61 kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2018 ambapo thamani ya mali za benki ilikuwa ni sh. billion 133.Jumla ya mikopo mwishoni mwa mwaka 2022 ilikuwa ni sh. 130.36 bilioni, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 4 ukilinganisha na sh. 125 bilioni mwaka 2021”
“Uwekezaji wa benki katika dhamana za serikali uliongezeka kwa asilimia 44 hadi kufikia sh. bilioni 41 bilioni kutoka sh. bilioni 28 mwaka 2021.”
“Amana za benki ziliongezeka kwa asilimia 11 kutoka sh. bilioni 150 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia shilingi 165 bilioni mwaka 2022, ongezeko hilo lilitokana na mikakati mahsusi ya benki ya kuongeza wigo wa huduma za fedha kwa wateja wake.”
“ Katika mwaka huo benki ilisherehekea tuzo kadhaa na kuibuka kinara katika Tuzo za ‘Consumer Choice Africa Award’ (CCAA), ikiibuka mshindi katika kitengo cha benki inayopendwa zaidi katika huduma kwa wateja Tanzania.
Benki vile vile ilishinda tuzo ya uwasilishaji wa taarifa bora za fedha inayotolewa na NBAA, katika kundi la benki za ukubwa wa kati, ikishikilia ushindi wa miaka mitano mfululizo katika tuzo hiyo,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Isidori Msaki.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi