March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Tabora aonya ubadilifu kwenye miradi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online-Tabora

MKUU wa Wilaya ya Tabora Upendo Wella amewataka wataalamu,watendaji na madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuongeza umakini kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali pamoja na kujiepusha na vitendo vya ubadhirifu.

Upendo ametoa onyo hilo wakati akiongea na wakuu wa idara,watendaji na madiwani wa halmashauri ya manispaa hiyo ambapo amewataka kuhakikisha miradi yote inasimamiwa ipasavyo ili ilete tija.

Amesema Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji miradi ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi katika manispaa hiyo ikiwemo ujenzi wa stendi mpya ya kisasa, soko kuu, barabara za lami za mitaa zenye urefu wa km 10 na mingine.

‘Simamieni ipasavyo miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yenu ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, kinyume na hapo tutakuwa na mashaka na weledi wenu,” ameeleza Upendo.

Pia amesema miradi yote inayotekelezwa na serikali ni ya wananchi, hivyo ikiwa chini ya kiwango viongozi waliopewa dhamana kusimamia miradi hiyo watawajibika.

Sanjari na hayo amewataka kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato pamoja na kubuni vyanzo vipya ili kuharakisha maendeleo ya wananchi, huku akimtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kutofumbia macho upotevu wa aina yoyote wa mapato.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, Hawa Mwaifunga, ameunga mkono maelekezo yaliotolewa na Mkuu huyo wa Wilaya huku akimhakikishia kufanya kazi kama timu na kufuatilia kwa umakini matumizi ya fedha zote zikiwemo zinazoletwa na serikali kuu.

Amesisitiza kuwa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) haiwezi kutekelezwa kama hakuna usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha za miradi, hivyo akaitaka timu ya mapato kufanya kazi kwa weledi.