Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Songea
Mkuu wa Wilaya ya Songea,Wilman Kapenjama Ndile, amewataka wananchi wa Songea kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuhamia kwenye nishati safi ili kutunza afya zao na mazingira na kuwa sehemu ya utekelezaji kwa vitendo mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unaolenga kuwafikia 80% ya watanzania ifikapo mwaka 2034.
Ndile ametoa hamasa hiyo wakati wa semina ya iliyofanyika mjini Songea leo, 10 Juni 2025,kwa wasambazaji wakubwa na wadogo wa gesi, maafisa biashara na afisa tarafa na wenyeviti wa mitaa.
“Huko nyuma tulitumia tani 40 za kuni kwa siku kupikia wafungwa wa gereza la Songea, leo tunajivunia kuwepo mkakati wa nishati safi ya kupikia, ambao Mhe. Rais anausimamia kidete na tunaona matunda yake, sasahivi tunatumia tani moja tu ya vumbi la makaa ya mawe kupikia, hivyo tunatunza muda,tunahifadhi misitu, tunapata hewa safi na tunatunza afya zetu.” Alieleza.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo vya mafuta na usambazaji wa gesi ya kupikia ili kuongeza wigo wa huduma kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kwa ujumla huku akitanabaisha kuwa mkoa huo una wasambazaji wakubwa watatu pekee wa LPG, hali inayochochea ufinyu wa huduma.
Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mha.Karim Ally, alieleza lengo la semina hiyo ni kuwaelimisha wadau hao kuhusu utaratibu wa leseni na vibali vya ujenzi vya vituo vya mafuta maeneo ya vijijini na biashara ya gesi ya kupikia baada ya EWURA kubaini uwepo wa uuzaji holela wa mafuta katika maeneo ya pembezoni na upungufu wa vituo vya kusambazia gesi ya kupikia katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
More Stories
Kiongozi wa Mwenge aifagilia RUWASA Tanga
Rais Samia kuanza ziara ya siku saba Simiyu na Mwanza
Msigwa awataka wazazi kuzungumza na watoto wao matumizi mabaya ya mtandao