May 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo atoa mwezi mmoja pikipiki za umeme zisajiliwe

Na Heri Shaaban,Timesmajiraonline,Ilala

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo,  ametoa mwezi mmoja kwa wamiliki wa pikipiki zote  za mizigo hususan zinazotumia umeme  maarufu kama maguta kusajiliwa rasmi Wilayani Ilala.

Mkuu wa Wilaya huyo ametoa agizo jijini hapa leo,Mei 22,2025 wakati wa mkutano na wamiliki wa vyombo hivyo 

“Natoa mwezi mmoja kwa pikipiki za umeme na maguta  zisajiliwe pia nawaomba waendesha pikipiki hizi muwe na leseni maalum za udereva na leseni ya usafirishaji kutoka Mamlaka ya udhibiti na usafirishaji kutoka Mamlaka ya udhibiti usafiri wa ardhini (LATRA)ikiwemo kuvikatia bima vyombo vyao,”amesema

Mpogolo amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la pikipiki hizo zinazotumia umeme katika maeneo mbalimbali na nyingi hazina bima wala namba za usajili,wala leseni madereva wake.

Pia amewataka waendesha pikipiki hizo kuwa na leseni maalumu za udereva na leseni ya usafirishaji  kutoka  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini ( LATRA) na kuvikatia bima vyombo vyao.

Aidha Mpogolo,ametaka vyombo hivyo kuthibitishwa ubora wake na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kutambua ubora wake.

Mpogolo amesema lengo ni kuhakikisha pikipiki hizo zina rasimishwa katika sekta ya usafirishaji kama ilivyo kwa bodaboda na bajaji,kuepusha ajali, kuwa linda madereva pindi wanapopata ajali kugharamiwa na bima pamoja na ukusanyaji mapato.

“Tunapenda afya zenu tunapenda uhai wenu. Vyombo hivi visajiliwe  vipate bima ili ukipata ajali ulipwe wewe na chombo chako na ni kwa mujibu wa sheria,”alisema.

Amesema baadhi ya vyombo hivyo vinasababisha ajali na dereva anayesababisha ajali hajulikani na chombo chake hakina usajili hivyo kuto kutambulika .

Aliongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali, ikiwamo LATRA,bima na Jeshi la Polisi watatoa elimu  kuhusu vyombo hivyo  kwa  majuma matatu kuanzia sasa.

Amesema dhumuni letu kuhakikisha vyombo hivi viwe katika utaratibu  Pia visiwe kero kwa wafanyabiashara wa Kariakoo na maeneo mengine bali viwe msaada kwa wafanyabiashara badala kuwa kero.