December 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mgomi awataka Watanzania kutambua kazi kubwa iliyofanyika kupatikana Uhuru

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Ileje

MKUU wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi, amewataka Watanzania kutambua kazi kubwa iliyofanyika hadi kupatikana kwa Uhuru Desemba 9, 1961 kwa njia ya amani.

DC Mgomi ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika kongamano la maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika,lililofanyika wilayani hapa, Desemba 9, mwaka huu.

Amesema Uhuru huo ulitokana na uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Aman Karume.

DC Mgomi amesema Watanzania wana kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa tunu kubwa aliyotupatia ya amani, mshikamano na upendo ambao Watanzania wamekuwa nao.

“Lakini hivi vitu havikuja kwa bahati mbaya, vimekuja kwa makusudi kutokana na uongozi madhubuti ulioanzia kwa mhasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Aman Karume,” amesema DC Mgomi na kuongeza;

“Wametujengea misingi imara ya upendo na mshikamano,ambapo sisi Watanzania ni wamoja hatujawahi kubaguana kwa misingi ya aina yoyote, iwe kwa misingi ya kabila, misingi ya dini, hata kwa misingi ya ukanda, hatujawahi kubaguana.”

Amesema Mwalimu Nyerere ametuletea mambo mengi ikiwemo lugha ya Kiswahili, huku wanawake wakiongozwa na mwanamke shupavu, Bibi Titi Mohamed, kupigania Uhuru

Amesema Bibi Titi Mohamed, alikuwa mwanamke wa kwanza ambaye alijitoa hata kuacha ndoa yake kwa ajili ya kupigania Uhuru, akishirikiana sana na Mwalimu Nyerere na kwamba yeye ndiye chimbuko la Jumuiya ya Wanawake.

“Yeye ndiye Mwenyekiti wa kwanza wa hiyo Jumuiya kabla
haijaitwa UWT, kwa kweli wanawake walifanya kazi nzuri, lakini pia vijana walifanyakazi nzuri na hiyo ilipelekea kuweza kupatikana Uhuru kwa amani kabisa,” amesema DC Mgomi.

Amesema kwa sasa Rais Samia Suluhu Hassan anayaendeleza kwa kiwango cha juu na kwa kiwango ambacho hakina mfano. “Yote tunatakiwa kuyatafakari katika dhana ya ushirikishwaji ambapo imeonekana ndiyo msingi wa maendeleo,” amesema.