December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mgomi ataka wahitimu Jeshi la Akiba kuwa macho ya Serikali

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Ileje

MKUU wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi, amehimiza wahitimu 174 wa mafunzo ya Jeshi la Akiba wilayani hapa kutumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko chanya katika jamii, ikiwemo suala zima la kuwa macho ya Serikali katika kuibua maovu katika jamii.

Aidha, amewataka wahitimu hao kutekeleza majukumu wanayopewa na viongozi wao ipasavyo.

DC Mgomi alitoa kauli hiyo Novemba 18,2024, aliposhiriki kufunga mafunzo ya Jeshi hilo la Akiba katika Kata ya Isongole wilayani hapa.

Aidha, DC Mgomi alitoa rai kwa wahitimu wote kushiriki kikamilifu katika suala zima la kutunza amani hasa kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Pia amewahimiza wahitimu hao kushiriki katika suala zima la ulinzi wakati wa uchaguzi huo, utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Katika hatua nyingine, DC Mgomi amewahakikishia wahitimu hao kuwa Serikali inatambua changamoto zilizopo hususan wakati wa mafunzo, hivyo kupitia Ofisi yake changamoto zimepokelewa kama zilivyoainishwa katika risala na kuahidi kufanyiwa kazi ili kuendelea kutambua nafasi ya Jeshi la Akiba katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Wahitimu wa mafunzo hayo walikuwa 174, ambapo wanaume ni 148 na wanawake walikuwa 26.