Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Songwe
MKUU wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi, amepongeza kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama ya Samia (Samia Legal Aid),kwani imeonesha umuhimu wa pekee wa kuongeza wigo wa ufikiaji haki kwa wananchi hususani walio pembezoni na ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili.
DC Mgomi ametoa kauli hiyo Desemba 12,2024,alipo mwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Godfrey Chongolo, kwenye uzinduzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani humu.
Amesema kampeni hiyo,imekuwa msingi mzuri wa kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria, jambo ambalo ni muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini.
Pia amesema kupitia kampeni hiyo migogoro mingi ya kifamilia na kijamii iliyodumu kwa muda mrefu imesuluhishwa,ambapo hali hiyo imeleta utengamano katika familia na tija katika jamii.
“Niwasihi wananchi wa Songwe kuitumia vema fursa hii ambayo nasi tumebahatika kuipata,” amesema DC Mgomi.
Amesema Wizara ya Sheria na Katiba imepewa dhamana ya kutekeleza majukumu ya Serikali yanayohusu masuala ya Katiba na Sheria za nchi, ambayo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya haki na utawala bora.
“Katika utekelezaji wa majukumu hayo, Wizara imeendelea kuzingatia miongozo mbalimbali ya kisera, kisheria, kikanuni na taratibu mbalimbali pamoja na maazimio ya kikanda na kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia katika kusimamia masuala ya haki na utawala bora,”amesisitiza na kuongeza;
“Majukumu hayo yanatekelezwa kwa kuzingatia dhima ya Wizara ya Sheria na Katiba,ambayo ni kuwa na mfumo madhubuti ya sheria na kikatiba katika kufanikisha utekelezaji wa sera na mipango kwa maendeleo ya Taifa letu,”.
Hivyo amesema,ni matarajio ya Rais Samia na Watanzania kwa ujumla kuona Wizara hii linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi na kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za kisheria kwa wakati na bila upendeleo wa aina yoyote.
“Sabamba hilo katika kuhakikisha nchi yetu inaongozwa kwa kufuata misingi ya haki, utawala wa sheria, utawala bora, Wizara pia imejipanga kutekeleza mkakati wa utoaji wa elimu ya sheria na utawala bora kwa viongozi katika ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa kuwajegea uwezo viongozi hao kuhusu haki na wajibu wao kikatiba, kuwaongezea uwelewa katika masuala ya haki za binadamu, uraia, utawala bora na demokrasia,”amesema
Amesema makundi yaliyokusudiwa ni kamati za ulinzi na usalama za mkoa na wilaya, wataalam wa halmashauri na watendaji wa kata zote za Mkoa wa Songwe.
Amesema kauli mbiu ya Mama ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inadhihirisha azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulinda, kukuza na kutetea haki za wanawake wanyonge na kupinga ukatili wa kijinsia, kulinda haki za binadamu na kuheshimu utawala wa sheria.
Ameongeza kwamba anaamini kuwa uzingatiaji wa haki za binadamu, utawala bora na utawala wa sheria ni msingi wa maendeleo ya nchi.
“Hakika kampeni hii inatekeleza falsafa ya Rais Samia ya 4R, kwani bila misingi imara utoaji haki ambayo ni majukumu muhimu ya Wizara ya Sheria na Katiba ni vigumu kutekeleza salsafa hii ya 4R,” alisema DC.
Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Songwe,ameeema wana furaha kwa maono ya Rais Samia kupitia kampeni hiyo.
Amesema msaada ya kisheria wa Mama Samia utaenda kutatua kero nyingi ambazo Wakuu wa Wilaya wamekuwa wakikabiliana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yao.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais