Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wafanyabiashara na wadau mbalimbali wametakiwa kuchangamkia fursa kwa kutumia bandari rasmi ya Tanga ili kuharakisha kupakia na kushusha mizigo yao kwa wakati
Aidha wametakiwa kuacha kufanya biashara ambazo si halali za magendo kwani zitakapokamatwa zitataifishwa .
Hayo ameyasema Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa wakati akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake ambapo amesema serikali ya Rais Dkt. Samia imejidhatiti kudhibiti magendo hayo kwa kutumia vyombo vya dola vinavyofanya kazi usiku na mchana.
“Wito kwa wafanyabiashara na wadau wengine mbalimbali, tunajua bandari yetu kwa mfano ya Dar es Salaam kwa kiwango kikubwa inawezekana ikawa imeelemewa mizigo ikawa mingi hivyo ni fursa watu kuanza kuitumia bandari ya Tanga ukifanya hivyo utaharakisha na kupakia kushuka na kushusha mizigo yako kwa wakati”
“Hivyo watanzania tuone umuhimu wa kutumia bandari ambazo ni rasmi na kuacha kufanya magendo” Amesema
Aidha Mgandilwa amesema Ujaji wa meli ya kushusha mizigo Tanga imechochea ongezeko la ajira kwa vijana lakini pia kuongeza fursa kwa wafanyabiashara wadogowadogo pia kupata kipato.
“Kuna vijana wetu wengi wamepata vibarua na kupata ajira kutokana na fursa hii iliyowekezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan”
“kuna mama lishe wa kitanga watauza vyakula vyao, kuna usafiri wa bodaboda n.k utatumika wa hapahapa Tanga hivyo kitendo cha uboreshaji wa miundombinu hii ya bandari inaakisi moja kwa moja maisha ya mwananchi wa chini”
Kwa upande wake Afisa masoko mwandamizi bandari ya Tanga, Rose Tandiko amesema mbali na Bandari kubwa ya Tanga mamlaka ya Bandari pia imeweza kurasimisha Bandari nyingine ndogondogo tatu katika mkoa na wilaya Zake, ikiwemo Bandari 2 kutoka Wilaya ya Pangani ambayo ni Bandari ya Kipumbwi na Mpaja pamoja na Bandari iliyopo katika Wilaya ya Tanga Mjini Bandari ya Sahare, ambapo bandari hizo ndogo tatu zimepelekea idadi ya kuwa na bandari ndogondogo nne ukijumlisha na Bandari ndogo nyingine kongwe ya Pangani.
“Zoezi la Urasimishaji wa Bandari hii umekua na matokeo chanya kwa mamlaka ya usimamizi wa Bandari kwani imewezesha biashara kati ya Tanga na Wilaya zake pamoja na upande wa visiwani kuwa nzuri na yenye tija na unafuu kwa wafanyabiashara”
“Wenzetu wa visiwani wanatutegemea sana kwa bidhaa nyingi kutoka Bara hivyo uwepo wa Bandari hizi zilizorasimishwa hasa hii ya Bandari ya Sahare iliyopo katika wilaya ya Tanga mjini imeweza kurahisisha biashara”
Naye mmoja wa wakazi katika bandari ndogo ya Sahare, Bwembe Idrisa amesema kuwa, kurasimishwa kwa bandari hiyo kumechochea ukuaji wa mapato yao kwani wafanyabiashara wanaoshusha bidhaa zao katika bandari hiyo wameongezeka.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato