December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mgandilwa aitaka jamii kutoa taarifa sahihi kwa Makarani wa Sensa

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

MKUU wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa ameitaka jamii kutoa taarifa sahihi kwa makarani wa sensa bila kuchanganya zoezi hilo na sababu za kisiasa wala kiimani.

Mgandilwa amesema ikiwa jamii itatoa taarifa zenye usahihi hata makarani wakifanya kazi hiyo kwa kiwango cha juu haitasaidia.

Hashim Mgandilwa ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya wakufunzi wa makarani 381 watakaoenda kufundisha makarani ngazi ya Halmashauri 11 za Mkoa wa Tanga.

Mgandilwa ameitaka jamii kutoa taarifa zenye ukweli na uhalisia katika maeneo yao kwenye zoezi la Sensa ya watu na makazi ili kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi zitakazoisaidia kujua na kupelekea huduma mbalimbali za kijamii kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa zima.

Aidha alisema kuwa utayari wa wananchi kutoa taarifa sahihi utasaidia kwa kiwango kikubwa kufanikisha zoezi Hilo litakalosaidia kuleta maendeleo ya kila mmoja na taifa kwa ujumla.

“Tunapozungumza habari ya sensa huwa wakati mwingine tunachukulia kama Jambo jepesi lakini ndio seh my sahihi ambayo itatumika kuratibu mipango mbalimbali kwa kipindi cha miaka 10 sasa katika kipindi hiki chote ni lazima upate takwimu sahihi kutokana na sensa ambayo tutaifanya sasa kwahiyo ni muhimu wananchi kutoa taarifa ambazo ni sahihi” alisema Mgandilwa.

Aidha Mgandilwa amewataka wakufunzi hao kwenda kufuata na kutumia miongozi ya kitaifa itakayotumika katika ukusanyaji wa taarifa kutoka kwa wananchi kama walivyoelekezwa katika Mafunzo yaliyofanyika kwa siku 21 huku akiwataka kuwa mstari wa mbele kuhamasisha kupitia njia mbalimbali kabla ya kuelekea siku hiyo ya augost 23, 2022 ikiwa ni pamoja na kuwasimamia makarani ipasavyo.

Katibu tawala msaidizi mkoa wa Tanga kitengo cha mipango na uratibu Abogust Kimasa aliwataka wakufunzi hao kwenda kufanya zoezi Hilo kwa weledi mkubwa ili kuzifanya mkoa wa Tanga kupata takwimu sahihi za pamoja na kuongeza katika zoezi hilo la kitaifa.

“Tanga tunaongoza kwa rasilimali zilizopo kwa ukubwa wa mkoa wetu Sasa majukumu haya mliyopewa mkayafanye kwa ufanisi , Hatutaki mkoa wa Tanga kuwa wa mwisho kitaifa nina imani baada ya mafunzo haya mliyopatiwa tutaongoza katika zoezi hili” alisema Kimasa.

Akizungumza mratibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 mkoa wa Tanga Tony Mwanjota alisema kuwa mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa njia ya tehama kwa mara ya kwanza tangu zoezi la sensa lianze hapa nchini wamejiridhisha katika utendaji wa wakufunzi waliohitimu Mafunzo hayo wote ambapo walifanya mitihani na kupata ufaulu aa jumla ya wastani wa asilimia 77.

“Mafunzo hayo yalilenga kuwa zoezi hili la sensa katika utumiaji wa vishikwambi halipati changamoto licha ya kuwa ni mara ya kwanza ni matarajio yetu kwamba washiriki watakwenda kufanya vizuri hii ni baada ya kufanya majatibio ya mitihani mitatu na kabla ya kupewa jukumu la kwenda kuwafundisha wengine na wastani wa ufaulu ilikuwa no asilimia 77 na kiwango cha juu cha ufaulu ni asilimia 92” alisema.

Zoezi hilo litafanywa Agosti 23 ikiwa ni mpango wa serikali wa kutaka kujua idadi kamili ya wananchi taarifa zitakazosaidia mipango mbalimbali ya maendeleo.