January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC.Massala:Tushirikiane kuwatafuta wanafunzi 275 ambao hawajaripoti kidato cha kwanza

Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

Jumla ya wanafunzi 275 sawa na asilimia 0.01,hawajaripoti shule kwa ajili ya kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kati ya 12,666 waliochaguliwa.

Ambapo kati yao wasichana ndio wameongoza kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawajaripoti wakiwa ni 152 huku wavulana wakiwa 123.

Hivyo wito umetolewa kwa Madiwani pamoja na watendaji mbalimbali kushirikiana kuwatafuta wanafunzi hao ili waweze kupata hali yao ya msingi ya elimu.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala,wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela cha robo ya pili ya mwaka wa fedha wa 2022/23, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo Februari 27, mwaka huu.

Ambapo ameeleza kuwa elimu ni kila kitu na ni kipaumbele kama taifa,mwanzo wakati wanaanza walipata changamoto upande wa sekondari hasa kwenye mahudhurio kwa kidato cha kwanza.

Ameeleza kuwa wamekuwa na jitihada kubwa ambayo wameifanya ndani ya Januari na Februari kwa ajili ya watoto ambao walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ambapo mpaka kufikia juzi takribani wanafunzi 275 hawajaripoti.

Pia ameeleza kuwa walitumia nafasi hiyo kufanya tathimini ya uandikishishaji kwa watoto wa shule za msingi.

Lakini mpaka sasa wana asilimia 99, ya wanafunzi wa kidato cha kwanza waliokuwa wanatakiwa kuripoti shule za sekondari kwa ajili ya kujiunga na wanaendelea na masomo.

“Mpaka kufika jana watoto 275, tu ndio ambao hawajaripoti shule ila wengine wote wapo darasani wanaendelea na masomo,mpaka kufika mwezi wa kwanza tulikuwa na asilimia 54 tu lakini mpaka tunamalizia mwezi Februari tumeisha fikisha asilimia 99,”ameeleza Massala

Hivyo amemueleza Ofisa Elimu Sekondari kuwaongoza katika suala hilo hili waone wanafika kwani wanahitaji watoto wote wa kitanzania lazima wapate haki yake.

“Natambua kuwa wapo ambao tumeisha pokea ripoti kuwa ni mjamzito kuna hatua tayari tumeisha zichukua lakini kuna hao wengine tunaomba tupate majina tushirikiane na Madiwani kuwatafuta,wito wangu Madiwani na watendaji wote ambao tunasaidiana kazi watoto hao waliobakia, tunao uwezo wa kuwaokoa na kuendelea kuwatafuta ili waweze kupata haki yao ya msingi,”.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Sylvester Mrimi, ameeleza kuwa mwaka huu walipangiwa wanafunzi 12,666 waliochaguliwa kujiunfa na kidato cha kwanza.

Hadi leo zaidi ya wanafunzi 12000 wa kidato cha kwanza,wameisha ripoti shule na wanaendelea na masomo huku
watoto 275 sawa na asilimia 0.01,hawajaripoti shule kwa ajili ya kujiunga na kidato cha kwanza kati yao wasichana 152 ambapo kati yao mmoja ndiye aliteripitiwa kuwa na ujauzito huku wavulana wakiwa 123.

“Asilimia 99.9 wameisha anza kidato cha kwaza na hao 275 ambao bado hawajaripoti tayari tumejipanga kuanza kuwasaka nyumba kwa nyumba, tunahitaji kila mtoto alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza anaingia shule,”ameeleza Mrimi.

Ameeleza kuwa wanatoa wiki moja watoto wote wawe shule kila mzazi au mlezi aweze kumleta mtoto shule na watawatumia watendaji na viongozi wa serikali ya mitaa kwani kuna baadhi ya wanafunzi Wana ujauzito na tayari wamechukua hatua kwa mamlaka za kisheria zinaendelea na hatua kwa yoyote aliye husika.

“Tayari tumepata kesi moja ya mtoto wa kike kupata ujauzito,na mamlaka za kisheria zimeishachukua hatua kwa ajili ya kumsaka aliye sababisha jambo hili na hatua zinaendelea kimsingi kila Mwananchi anatakiwa kutambua kuwa mwanafunzi analindwa na sheria ya nchi kwa ana haki ya kuhakikisha kwamba anapata elimu,”.