December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Ludewa atoa maelekezo matumizi ya kipikipi nane

Na Mary Margwe,TimesMajira Online, Ludewa

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe Victoria Mwanziva amekabidhi pikipiki kwa maafisa watendaji wa kata 8 zilizotolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwataka watendaji hao kuzilinda kikamilifu ili kutimiza lengo la Mh.Dkt.Samia katika kuboresha na kuwarahisishia utoaji wa huduma kwa jamii.

Akikabidhi piki piki hizo kwa watendaji hao 8 juzi, Mwanziva amemshuru Mh.Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan kwa kutoa vyombo hivyo vya usafiri vitakavyo warahisishia watendaji kufanya kazi zao kikamilifu kutokana na jiografia ya maeneo mbali mbali ndani ya Wilaya ya Ludewa.

Alisema Dkt.Samia aliahidi na sasa ametekekeza kutoa pikipiki kama vifaa vya usafiri kwao, hivyo wanapaswa kuvitunza vifaa hivyo ili viwafae katika kazi zao kwa muda mrefu zaidi na hatimaye kuleta ufanisi katika Utekelezaji wa majukumu yao.

” Ninaomba Watendaji wote wanane mliokabidhiwa pikipiki siku ya leo kuhakikisha mnalinda imani kubwa aliyo wapa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa kuwaletea pikipiki zitakazo wasaidia katika majukumu yaenu ya kazi ” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha alisema imani hiyo italindwa kwa matumizi mazuri ya hivyo vifaa kwani Mheshimiwa Rais aliahidi, na ametenda hivyo ahakikisheni mnavitunza kikamilifu vifaa hivyo ili viwafae katika kazi zao kwa mda mrefu.

Pia aliwatahadhalisha watendaji hao kuhakikisha wanazitumia pikipiki hizo katika kazi zilizo kusidiwa na kuboresha ufanisi wa utendaji wao, na si vinginevyo.

” Halmashauri ya Ludewa ina jumla ya Kata 26, lakini watendaji wa Kata wanane ndio mliofanikiwa kupata usafiri, hivyo hakikisheni mnaboresha utendaji wenu wa kazi uwe wa ufanisi katika jamii, yaani mnatakiwa mtuonyeshe utofauti wa sasa na wakati ule mlipokua hamjapata usafiri, tuone mabadiliko chanya baada ya kupata vyombo vya usafiri” alisisitiza Victoria Mwanziva Mkuu wa Wilaya ya Ludewa.

Mmoja wa watendaji waliopata pikipiki hizo wa Kata ya Madope Maria Ngatunga alimshukuru Mh. Rais Samia kwa kuwapatia usafiri huo na hivyo kuahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa uhadirifu wa hali ya juu.

Aidha alisema kwa kupata usafiri huo, wanaahidi kuwahudumia wananchi kwa kasi kubwa zaidi ya jana ukilinganisha na siku za nyuma walipokua hawana usafiri, hivyo watarajie mabadiliko na mafanikio makubwa zaidi.

” Mkuu wa Wilaya nikuhakikishie na nikuondoe hofu kwa kupata pikipiki hizi mlizotukabidhi Leo hii zinakwenda kuongeza ufanisi katika utendaji wetu wa kazi, jambo la kufanya siku nzima sasa tutalifanya kwa kutumia saa moja, tunamshukuru sana Mama yetu, mama wa Wanzania, Mama mpambanaji wetu Samia Suluhu Hassan na tunaahidi kuwahudumia wananchi kwa kasi kubwa sasa” alisema Maria Ngatunga Mtendaji wa Kata ya Madope mmoja wa wapokeaji wa pikipiki hizo.

Hata hivyo Mwanziva aliongeza kuwa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa ni miongoni mwa Halmashauri nchini iliyopata pikipiki 8 kati ya pikipiki 916 zilizotolewa na serikali na kuzigawa kwa Maafisa Watendaji wa Kata.