Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Njombe
MKUU wa Wilaya ya Njombe mkoani Njombe Kissa Kasongwa amewahamasisha Watanzania waweze kutembelea wilaya hiyo ili kuona vivutio vya utalii, ambapo kuna utalii wa baridi, kupanda farasi na kuona Mto Hagafilo ambao ni kama nyoka anaetembea kwa kujikunjakunja.
Lakini pia kuna maeneo yenye nyasi fupi ambayo watu wanaweza kufanya sherehe mbalimbali ikiwemo siku ya kuzaliwa, harusi na ubarikio pembezoni mwa Mto Hagafilo.
Aliyasema hayo Julai 16, 2022 alipofika kufanya utalii wa ndani kwenye Kata ya Uwemba, ambapo alifika Parokia ya Uwemba ambayo ipo ndani ya Shirika la Mtakatifu Benedict kwa ajili ya kupanda farasi.
“Nawaalika Watanzania wote kuweza kufika Wilaya ya Njombe ambako kuna utalii wa aina nyingi ikiwemo wa baridi. Wilaya ya Njombe huwa inafikia baridi ya Nyuzi Joto tano mpaka 10, na kufanya maeneo mengine kuwa na barafu.”
“Lakini kuna maeneo mengine kama kupanda farasi waliopo Parokia ya Uwemba, Kanisa Katoliki. Farasi hawa ni kivutio kwenye wilaya yetu, hivyo watu wengi wamekuwa wakifika hapo kupanda farasi hao” alisema Kassongwa.
Kassongwa alisema, pembeni ya farasi hao, kuna mandhari nzuri ya Serikali kwenye Kata ya Uwemba, ambapo watu wanaweza kusheherekea siku yao ya kuzaliwa, harusi ama ubarikio. Kwani eneo hilo, kuna Mto Hagafilo, ambao upinda kona nyingi.
“Ukiacha farasi, kuna Ikolojia inayovutia zaidi. Kuna Mto Hagafilo ambao umepindapinda kama nyoka anaetembea. Lakini pembeni yake kuna nyasi fupi fupi ambazo ni za asili, watu wanaweza kutumia eneo hilo kufanya utalii, huku wakiwa na shughuli zao mbalimbali kama ubarikio, harusi au birthday” alisema Kassongwa.
Muongoza wageni wanaokwenda kupanda farasi, Bruda (Brother) Kizito Nsafiri kutoka Shirika la Mtakatifu Benedict, alisema anashukuru kutembelewa na Mkuu wa Wilaya Kissa Kasongwa, na kusema yeye ndiyo kiongozi wa kwanza wa Serikali kuhamasisha utalii kwenye Parokia ya Uwemba, na eneo lote la Uwemba.
Yeye ndiyo kiongozi wa kwanza wa Serikali kupanda farasi. Tumefarijika sana kuona Mkuu wetu wa wilaya anahamasisha utalii Kata ya Uwemba.”
“Ukiacha farasi, kata yetu ya Uwemba ina maeneo mengi ya utalii ikiwemo Mto Hagafilo ambao umejikunja kama nyoka anaetembea, na una maji wakati wote, sababu juu ya mto huo kuna misitu minene, hivyo ni eneo zuri kwa kufanya utalii” alisema Bruda Kizito.
Parokia ya Uwemba ni nyumba ya Kitawa ambamo wanaishi Watawa wa Shirika la Wamisionari Wabenediktini wakiwemo Mapadre na Mabruda.Parokia ya Uwemba ilianzishwa Januari 23, 1931 na Padre Yosef Damm wa Shirika la Mtakatifu Benedict.
Na farasi waliopo hapo ni kwa ajili ya kupanda hasa wageni wanaoitembelea kama kivutio Uwemba Misheni, Pia wanauza kwa wale wanaohitaji, lakini hasa ni utalii wa ndani.
More Stories
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi