November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dc Joketi aja na mbio za wajawazito Korogwe

Na David John,Timesmajiraonline,Korogwe

NI Mei 28 Korogwe! Hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea tukio kubwa la mbio za wanawake wajawazito ambazo zitafanyika siku hiyo wilayani Korogwe mkoani Tanga ambapo lengo ni kuokoa afya za wanawake ndani ya wilaya hiyo.

Akizungumza Mei 25, 2023 mbele ya waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo mbio hizo za wanawake wajawazito zinaitwa ‘Mamathon’ huku akitumia nafasi hiyo kueleza kauli mbiu itakayotumika ni Mwendo wa Mama.

“Mbio hizi ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya Wanawake wajawazito zitafanyika Mei 28 mwaka huu na zitaanzia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe na kuelekea viwanja vya shule ya msingi ya Mazoezi.Maandalizi kwa ajili ya Marathon hizi yamekamilika na itakuwa ya aina yake.”

Ameongeza lengo kubwa la Marathon hizo ni kuendelea kuhamasisha wanawake wajawazito kuachana na dhana potofu wanazozipata wakati wanapokuwa wameba ujauzito. “Tumekuwa na marathon nyingi ambazo tumeshuhudia lakini hii ya Wanawake wajawazito ndio inakwenda kufanyika kwa mara ya kwanza.

” Na tunaifanya hapa Korogwe, njooni mshuhudie akina mama wajawazito wanavyoshinda kukimbia.Nikiri kwa kutambua mwendo wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo tumeona kama viongozi tuna wajibu wa kuwakutanisha jamii na kuyaenzi yale serikali yanayofanya, “amesema Jokate.

Akifafanua kuhusu kauli mbiu hiyo amesema inatafsiri nyingi ambayo ni ule mwendo ambao ameuanza Rais Samia kwa namna anavyowaongoza katika nchi kuwa na maendeleo.” Kauli mbiu yetu ya mwendo wa mama ni kutambua mchango wa Rais Samia namna anavyoitumikia Tanzania, anavyogusa kundi la akina mama kwenye kila pembe ya nchi yetu.”

Aidha amesema mbio hizo pia zinawahusu wanawake wote, hivyo ni muhimu kujiandikisha katika vituo vya afya na hospitali ili takwimu kamili ipatikane na wale wajawazito watapatiwa zawadi kwa ajili ya kuwasaidia kujifungua salama huku akieleza ili kuandaa zawadi hizo ni lazima wapate idadi ya wanawake hao kwa ajili ya maandalizi ya siku hiyo muhimu.

Pia amesema kwamba wakati wa mbio hizo watatoa elimu ya afya ya uzazi na lishe lengo ikiwa ni kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa afya njema na watazindua lishe bora ili vizazi vinavyozaliwa vitakuwa na lishe nzuri na akili timamu hivyo kushiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi hii.