January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Jokate Mgeni rasmi jukwaa la Irada Style

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika jukwaa la wanawake lililoandaliwa na Irada Style ambalo litamsaidia mwanamke kutimiza malengo yake kupitia mavazi na muonekano wake.

Lengo la kukutana pamoja wanawake hao wabunifu ni kuendelea kusherehekea siku ya wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 8 Machi, kwa kuonyesha bunifu zao mbalimbali ikiwemo kufanya mnada wa nguo.

Fedha zitakazopatikana kupitia mnada huo zitaenda kusaidia vituo vya watoto yatima na wale wasiojiweza katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo, Muanzilishi na mmiliki wa Irada Style, Irada Mahadhi amesema Jukwaa hilo litafanyika Machi 17 saa 12 jioni hadi saa 4 usiku katika Hoteli ya Hyatt Jijini Dar es Salaam kutakua na uzinduzi wa fashion show ya Ramadhan na Eid Collection ambayo kila mwaka huwa wanaizindua.

“Wakati tunaanzisha Irada Style, lengo letu kuu ni kuwasaidia mabinti wote wakike ambao wanapenda kuonekana wamependeza katika mavazi yakistaarabu”

“Tutazindua fashion show ya Ramadhan na Eid Collection ambapo tutawachagua wanawake ambao tumeweza kuwapa ujuzi katika muda wa mwaka mzima kutimiza malengo yao ya kibiashara hususani kuwapa fursa tofauti, ikiwemo katika upande wa ubunifu wa mavazi na mitindo,” amesema Mahadhi.

Mahadhi amesema, jukwaa hilo litahudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka serikalini na taasisi tofauti lakini pia wafanyabiashara.

Aidha Mahadhi amesema, tiketi zinapatikana katika duka lao la Dar Free Market, Ilala na Kinondoni kwa shilingi 85,000/= za kitanzania

Pia Mahadhi amewakaribisha wadau wote kushiriki katika jukwaa hilo ili Kuwaunga mkono wabunifu hao kupitia kazi zao.