November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Itunda atupiwa fupa la wakulima na wafugaji

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo,
amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda, kutambua mifugo yote iliyoingizwa Wilayani humo bila vibali ili walioruhusu wachukuliwe hatua kali sanjari na mifugo hiyo kurejeshwa ilikotoka.

Pia amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya kuweka zuio la mifugo mingine kuingizwa katika Wilaya hiyo ili kuepusha kuibuka kwa migogoro ikiwemo kupata suluhisho la kudumu la migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Chongolo ametoa maelekezo hayo, Mei 28, 2024 baada ya kupokea malalamiko ya wakazi wa kijiji cha Iseche katika Mwambani, Wilayani humo kulalamikia tabia za wafugaji kulisha mazao yao na kusababisha tishio la ukosefu wa chalula kwa wananchi.

“Mimi ni muumini wa utaratibu na niseme tuu hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwenye hili nataka ili kulimaliza ni lazima uanze na wale wanaowakaribisha hao watu (wafugaji), mimi sitaki kusikia tena migogoro ya wakulima na wafugaji… narudia sitaki kusikia tena migogoro ikiendelea kati ya wakulima na wafugaji katika Wilaya hii” Mkuu wa Wilaya ( Itunda) umenielewa?amehoji.

Awali akijibu kero za wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Songwe,Solomon Itunda licha ya kukiri kuwepo kwa migogoro ambayo alidai kuwa ni ya muda mrefu,amesema kuwa tayari wameshaanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuunda timu ndogo ya kuratibu utatuzi wa migogoro hiyo.

Ameeleza kuwa pamoja na majukumu mengine, timu hiyo ambayo aliiunda Mei 15 mwaka huu itakuwa na jukumu la kufanya doria za mara kwa mara katika wilaya hiyo.

Itunda ameeleza kuwa tayari baadhi ya wafugaji ambao wanatuhumiwa kuhusika na kulisha mazao wa wananchi wameshakamatwa na hutua zingine zinaendelea.

Hatua nyingine ambao DC Itunda amesema wamekubaliana ni kuimarisha sungusungu kila kata.