January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Ilala akabidhi majiko,mitungi ya gesi kwa mama lishe

Na Agnes Alcardo,Timesmajira Online. Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo Machi 22, 2024 amekabidhi majiko na mitungi ya gesi 18 kwa mama lishe walioonekana kufanya vizuri katika utoaji huduma za chakula kwa kufuata viwango vya mlo kamili na usafi wa mazingira wilayani humo.

Majiko hayo ameyatoa katika mafunzo na maonesho ya Mamalishe wa Wilaya hiyo, yaliyokuwa na kauli mbiu ya ” Wekeza katika nishati safi ya kupikia na mazingira” huku kati ya hayo  majiko ya gesi madogo 13 na mitungi mkubwa ya gesi mitano.

Mafunzo hayo, yalikuwa na lengo la kutoa elimu kwa mama lishe hao juu ya  kuzingatia makundi ya vyakula na usafi kwa ujumla kwa maslahi mapana ya walaji, huku Mkuu wa Wilaya, Mpogolo, akiwataka kuanzisha umoja wao, ili waweze kunufaika na mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri.

” Mama lishe ni mtu muhimu katika jamii yetu na anapaswa kuheshimiwa, nyie ni mama zetu, dada zetu na hata shangazi zetu, mnajitafutia riziki kupitia kazi hii kwa ajili ya kuendesha familia zenu,ni vyema mkaenda kuyafanyia kazi  mafunzo mnayopewa hapa kuhusu utoaji huduma hii ulio bora zaidi,”amesema Mpogolo.

Pia Mpogolo amewaondoa hofu mama lishe hao na kudai kuwa, Serikali inaenda kushughulikia changamoto zote wanazokabiliana nazo ikiwa  ni pamoja na kukarabati maeneo yasiyo rafiki katika shughuli zao za upishi.

Kwa upande wake Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Neema Mwakasege,amewasisitiza mama lishe hao juu ya kuzingatia upishi wa makundi sita ya vyakula, ili kuwaepusha walaji na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama shinikizo la damu na kisukari.

Amesema, Halmashauri hiyo tayari imeshatoa mafunzo kwa mama lishe 1500 juu ya usafi na usalama wa chakula pindi kinapoandaliwa.

Pia amesisitiza juu ya kuongeza kiwango cha mbogamboga kwa walaji na matunda ili kumlinda kiafya.

Mafunzo hayo yameandaliwa na benki ya NMB Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ilala na kushirikisha mama lishe kutoka Kata 36 za wilayani humo.