January 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Gondwe: Serikali kufanya maboresho ya sheria ya habari

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Serikali kupitia wizara ya habari inafanya maboresho ya sheria ya huduma ya vyombo vya habari na taasisi za habari kwa lengo la kuhakikisha kunakua na sheria bora itakayowawezesha wanahabari kupitia taaluma yao kufanya kazi zao vizuri kwa uhuru kwa manufaa yao, jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo ameyasema Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe wakati wa mahafali ya 27 ya chuo cha uandishi wa habari (DSJ) leo jijini Dar es Salaam.

DC Gondwe amesema serikali itaendelea kusimamia changamoto iliyopo sasa katika eneo la utoaji na upashanaji habari hasa katika masuala ya utandawazi kwa kutolewa miongozo na sheria mbalimbali.

“Serikali inatambua changamoto kubwa iliyopo sasa kwenye eneo la utoaji na upashanaji wa habari hasa katika masuala ya utandawazi na uwepo wa mitandao ya kijamii ambapo kumekuwepo na watoa taarifa wengi wasio rasmi hivyo kupotosha hivyo serikali itaendelea kusimamia suala hili”

Pia DC Gondwe amesema serikali inaendelea kuhakikisha kwamba mwanahabari analindwa na kuthaminiwa katika kazi zao.

“Mipango inaendelea kuhakikisha kwamba taaluma ya uana ya habari na upashaji wa habari na wanahabari wanatambuliwa na wanathaminiwa na wanalindwa katika kazi zao kisheria”

Mbali na hayo, DC Gondwe aliwahisi wahitimu kufanya kazi kwa misingi ya taaluma na maadili ya kazi zao kwa kufuata sheria za nchi ya Tanzania.