January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Gondwe azindua wiki ya utafiti na ubunifu DUCE

Na Mwaandishi Wetu, TimesMajira online, Dar

MKUU wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe amezindua maonesho ya wiki ya Utafiti, Ubunifu na ugunduzi kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu Kishirikishi cha Elimu (DUCE) Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe akizungumza na wanataaluma, wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) wakati wa uzinduzi wa wiki ya utafiti na ubunifu iliyoandaliwa na chuo hicho na kuwapongeza kwa jitihada wanazozifanya za kupeleka tafiti hizo kwa jamii.

Maonesho hayo yanafika kwa mwaka wa sita, yanahusisha utafiti wa vitu mbalimbali, machapisho na ugunduzi unaofanywa na wanataaluma kutoka chuo hicho.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jana,Gondwe amesema ni furaha kuona Wilaya ya Temeke wanafanya mambo makubwa ikiwemo masuala ya utafiti kwani kwa dunia ya sasa inahitaji teknolojia ili twende kwenye maendeleo zaidi.

Dkt. Mabula Nkuba kutoka Chuo Kikuu Kishiriki Dar es Salaam (DUCE) akitoa maelezo ya moja ya tafiti waliyoifanya Kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu kwa wanataaluma wa Chuo hicho inayofanyika kwa Mwaka wa sita

Gondwe amesema, wanataaluma wameonesha ukomavu mkubwa sana katika kufanya tafiti hizi na zenye malengo ya kimkakati kwa jamii ukizingatia zina tija katika kukuza sekta ya teknolojia.

“Nimeona utafiti mzuri sana uliofanywa na wanataaluma hawa ukiangalia programu iliyobuniwa itasaidia katika kupunguza changamoto za utoro kwa wanafunzu,” amesema.

Rasi wa Chuo Kishirikishi cha Elimu Tanzania (DUCE) Prof Stephen Maluka amesema lengo kuu la maonesho haya ni kuonesha tafiti,ubunifu na ugunduzi wa taaluma kutoka kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).

amesema, Wiki ya utafiti,bunifu na ugunduzi inafanyika kwa mwaka wa sita na wanataaluma wanapewa nafasi ya kuonesha tafiti mbalimbali walizozifanya ndani ya mwaka mzima.

Rasi amesema “wanataaluma hao wanapata nafasi ya kuonesha tafiti zao na machapisho wanazozifanya Kila mwaka na hii inafanyika kwa mwaka wa sita”

Rasi Maluka amesema, kabla ya kuanza kwa maonesho haya
Tafiti nyingi zilizopaswa kusaidia jamii hazikuwa zinawafikia walengwa kutokana na kutokuwekwa hadharani na kuishia kukaa maktaba.

Maluka ametoa wito kwa wadau mbalimbali kufika katika maonesho hayo kuangalia, kujifunza kushirikiana nao katika tafiti hizo zenye tija kwa taifa.

Aidha, amesema tafiti hizo zimeweza Kukitangaza chuo na wanatafiti watashindanishwa, washindi watatu wataenda kushindanishwa na wanatafiti wengine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na baada ya hapo watapatiwa tuzo ili kutambua mchango wao katika tafiti.

Moja ya watafiti hao Dkt Mabula Nkuba amesema walifikia maamuzi ya kuunda programu itakayosaidia walimu kuwasiliana na wazazi kwa njia ya mtaalndao baada ya kuona changamoto mbalimbali zikiendelea kujitokeza na wanafunzi wengi wakishindwa kuendelea na masomo.

Nkuba amesema wameanza na shule mbili na mwitikio umeonekana mkubwa walimu na wazazi wakipendezewa na programu hiyo na wamejizatiti zaidi kuzifikia shule nyingi zaidi hususani za serikali.

Tafiti hizo zimekuwa na muendelezo mzuri na DUCE wamewataka wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuja kutembelea mabanda yao ndani ya Viwanja vya Chuo chao kuanzia Aprili 27-29 na washindi watakaopatikana hapo wataenda kushindanishwa na watafiti wengine kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).