Na Judith Ferdinand, Timesmajira online, Ukerewe
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Hassani Bomboko amesisitiza wajibu wa usimamizi wa familia kwa kila mmoja ili kuimarisha maadili na upendo katika familia.
Hii ikiwa ni njia moja ya kuiishi kwa vitendo kauli mbinu ya maadhimisho ya siku ya familia duniani kwa mwaka 2023,inavyosema “imarisha maadili na upendo kwa familia imara”
Bomboko amezungumza hayo katika maadhimisho ya siku ya familia dunia ambayo uadhimishwa kila ifikapo Mei 15, ambapo kwa Wilaya ya Ukerewe,wameadhimisha kwa kufanya mdahalo uliowahusisha viongozi mbalimbali wa serikali, dini,wananchi na wanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari Bukongo huku mgeni rasmi akiwa Mkuu huyo wa Wilaya.
Ambapo ameeleza kuwa ili kuwa na familia zenye maadili na upendo serikali inapendekeza wanafamilia ikiwahusisha baba,mama,watoto, ndugu na jamaa kukaa pamoja ili kujadili mafanikio katika familia.
Na kujadili changamoto zilizopo ili kutafuta majibu ya pamoja kwa amani na upendo ili kuendelea kudumisha mshikamano na maelewano ndani ya familia na jamii yote kwa ujumla.
Ameeleza kuwa madhumuni ya siku hiyo ni kuhamasisha, kuhimiza,kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa familia katika jamii kwa nia ya kuchukua hatua zinazopaswa ili kuziimarisha na kuziendeleza.
Sanjari na hayo ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi na viongozi wa dini kutoa mafundisho mema kwa jamii juu ya masuala mbalimbali ikiwemo ya kushiriki vyema shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Pamoja na kukemea masuala ya ushoga, kupinga uvuvi haramu,kuhimiza wazazi hususani baba kufahamu wajibu wao katika kuijenga familia bora na jamii iendelee kudumisha amani katika Wilaya ya Ukerewe.
“Tunakumbushwa wazazi na walezi kutambua wajibu wetu wa msingi juu ya malezi ya watoto na familia hasa kwa akina baba kujua wajibu wao kama wazazi au walezi kwa Watoto katika maeneo makuu 3 ya msingi ambayo ni kumjali mtoto katika maeneo ya msingi, kumlinda mtoto dhidi ya ukatili na kuzungumza na mtoto mara kwa mara ili kufahamu changamoto zinazomkabili na maendeleo yake kwa ujumla,”ameeleza Bomboko.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Emmanuel Sherembi amewasisitiza wananchi wote kutokomeza masuala ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wazazi kutoa elimu sahihi kwa watoto ili kuondoa tatizo la watoto wa mtaani.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Ukerewe Eliarusia Nassary amewataka wazazi kujenga msingi bora kwa watoto kwa kuwapeleka shule na kufuatilia mienendo yao, wazazi kushirikiana katika malezi ya watoto na wahusike kupinga mila potofu zinazo ikandamiza jamii ili kuwajengea uwezo vijana watakao saidia kuchochea maendeleo katika nchi yao.
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ukerewe Nasra Msuya amefafanua kuwa suala la malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wazazi na walezi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwalea watoto hao ili kuwa na kizazi bora na imara kwenye familia.
Huku akisisitiza kuwa wazazi na walezi watenge muda mwingi wa kukaa na watoto wao ili wajadili changamoto na kuzitatua.
Aidha Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ukerewe Wanchoke Chinchibera amehimiza wazazi kuendelea kuboresha maadili ya watoto kwa kuwahusisha katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo,ujasiliamali na uzalendo kwa nchi yao.
Mmoja wa wananchi waliohudhuria mdahalo huo Happy Magesa, amesema kuwa familia nyingi za kitanzania zinakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na uwepo wa mila na desturi zenye kuleta madhara, umaskini uliokithiri, mawasiliano na miundombinu mibovu ambayo husababisha hali ya maisha ya watu kuwa duni na tegemezi na hatimaye kutumia muda mwingi wa kufanya kazi bila ya kujali madhara yatakayotokea kwa familia.
Ambapo ameeleza kuwa miongoni mwa madhara hayo ni pamoja na watoto kuwa na tabia mbaya kama kuacha shule, kukimbilia mitaani, kutokuwa na maadili na kuiga tamaduni zisizokubalika katika jamii nchini
“Ni wazi kuwa changamoto hizi zinaweza kushughulikiwa vyema kuanzia ngazi ya familia na ngazi mbalimbali za uongozi, napenda kuwaasa wazazi wenzangu kutenga muda wa kutosha kukaa na familia zao ili kujadili, kushauriana na kutekeleza masuala muhimu ya kuendeleza familia zao kwani familia ndiyo kitovu cha maendeleo,”.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango