November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC awaka kutoridhishwa ukusanyaji mapato ya ndani

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga William Mwakilema amesema haridhiki na ukusanyaji Mapato ya Ndani kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji Korogwe.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ilijiwekea lengo la ukusanyaji Mapato ya Ndani ya zaidi ya bilioni 3.1 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 lakini mpaka Oktoba mwaka huu wamekusanya zaidi ya milioni 749 sawa na asilimia 24, wakati kwa miezi hiyo minne (4), walitakiwa wawe wamekusanya mapato kwa asilimia 33 sawa na zaidi ya bilioni 1.02.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema akihutubia Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe

Amesema hayo wakati anahutubia Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa huo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe.

“Ukusanyaji wa mapato kwa mwaka 2023/2024 kwa Halmashauri ya Wilaya na Mji ni hafifu,bado tupo chini, hivyo tuongeze mapato tulipanga kukusanya zaidi ya bilioni 3.1,hadi sasa tuna asilimia 24 wakati tulitakiwa tuwe na asilimia 33 ,tupo njia kuu (Dar es Salaam- Arusha- Nairobi), kwa nini tusifikie malengo kama wengine, wakati kwa wenzetu waliopo pembezoni wanakusanya fedha nyingi,”amesema.


Hivyo kama kuna mchwa wadhibitiwe
Korogwe wana mazao ya chakula na biashara haiwezekani washindwe kufikia malengo ya ukusanyaji mapato.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe akizungumza kwenye Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mhidini Rajabu (kushoto), na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe David Mpumilwa (kulia)

Mwakilema ambaye kabla ya uteuzi huo, alikuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), amesema kuna baadhi ya miradi ni viporo kwa muda mrefu ikiwemo maabara zilizojengwa kwenye shule za sekondari za kata tangu mwaka 2014, hivyo ametaka iwekewe mikakati ya kukamilisha.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe amesema ukusanyaji mapato lazima uongezeke, na sio kuishia kwenye mifuko ya watu.

“Wakati mwingine POS (mashine ya ukusanyaji mapato kwa kielektroniki) haisomi, inakuwa imezimwa na kujikuta fedha hazifiki kwani kama mashine hiyo ilikuwa ikusanye 250,000 au 500,000, fedha hiyo haiwezi kufika serikalini na zinakuwa zimepotelea kwenye mifuko ya watu,” amesema Kallaghe.

Kallaghe amesema utekelezaji wa miradi bado hauridhishi hivyo ameiagiza Menejimenti ya Halmashauri kukamilisha miradi ifikapo Desemba 31, mwaka huu ikiwemo jengo jipya la Utawala la Halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, na Katibu wa Madiwani wa CCM Selemani Mwongozo (kushoto), Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji Emmanuel Mng’ong’ose (kulia), na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Uchumi na Mazingira Idd Shebila (katikati), wakiwa kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe

“Tunaiagiza Menejinenti ya Halmashauri iwe imekamilisha miradi ifikapo Desemba 31, mwaka huu sipendi wala rushwa, wazembe na wasiowajibika. Tusilazimishane kuingia kwenye ugomvi,”amesema Kallaghe.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wakiwa kwenye kikao